Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni

Tunaipa Uhai wa Kisheria Biashara yako

Habari

WATUMISHI WAPYA BRELA WAPATIWA MAFUNZO ELEKEZI


 

WATUMISHI WAPYA BRELA WAPATIWA MAFUNZO ELEKEZI

Watumishi wapya wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), wanashiriki katika mafunzo yenye lengo la kuwapatia maarifa na ujuzi utakaowasaidia katika utendaji kazi za BRELA.

Mafunzo hayo yanayofanyika kwa siku sita yameanza leo tarehe 4 na kuhitimishwa tarehe 11 Desemba, 2023 katika Ukumbi wa Chuo cha Utumishi wa Umma, jijini Dar es Salaam.

Mkuu wa Chuo na Mtendaji Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Dkt. Ernest Mabanesho, Katika ufunguzi wa mafunzo hayo ameipongeza BRELA kwa kutekeleza wajibu wao katika kutimiza takwa la kisheria ambalo linawataka watumishi wote wapya katika utumishi wa umma wapewe mafunzo mara tu wanaporipoti katika vituo vyao vya kazi.

Mkuu wa Chuo ameeleza mada mbalimbali zitakazowasilishwa kwa watumishi hao kuwa ni pamoja na Maadili, Sheria na Kanuni za Utumishi wa Umma, Muundo wa Serikali na Uendeshaji wa Ofisi, Utunzaji wa Nyaraka na Kumbukumbu, Huduma bora kwa Mteja na UKIMWI na magonjwa yasiyoambukiza.

Pia Mkuu huyo amesisitiza kuwa watumishi hao wanapaswa kuzingatia maadili na kanuni mbalimbali za Utumishi wa Umma.

“Maadili ni msingi muhimu wa utendaji bora wa kazi na tunatarajia kila mmoja wenu atazingatia maadili haya katika utumishi wenu. Sheria na kanuni za utumishi wa umma ni muhimu katika kuongoza matendo yetu na kuhakikisha uwajibikaji na uwazi katika utendaji wetu wa kazi,” amefafanua Dkt. Mabanesho.

Amewataka pia watumishi kuwa makini wakati wa mafunzo kwani yatajumuisha sheria na taratibu za BRELA.

“Nimuhimu kufahamu na kuzingatia sheria na taratibu zetu ili kuhakikisha utendaji wa kazi unaofuata miongozo, taratibu, kanuni na sheria,” amesema Dkt. Mabanesho

Mafunzo hayo yanahudhuriwa na watumishi 56, ikiwa pamoja na watumishi 16 wa ajira za kudumu, watumishi nane (8) waliohamia BRELA, ajira za mkataba 25 na watumishi saba (7) wanaojitolea kutoka Wakala wa Huduma za Ajira Tanzania (TAESA).