Habari
BRELA YAPONGEZWA KUBORESHA HUDUMA KWA NJIA YA MTANDAO-MHE. KIGAHE
BRELA YAPONGEZWA KUBORESHA HUDUMA KWA NJIA YA MTANDAO-MHE. KIGAHE
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe.Exaud Kigahe(Mb) ameipongeza Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), kwa juhudi za kufanya maboresho ya huduma za sajili na utoaji wa leseni kwa njia ya mtandao kupitia mifumo ya Usajili kwa njia ya Mtandao (ORS) na dirisha la Taifa la biashara (TNP).
Mhe.Kigahe amebainisha hayo wakati akimuwakilisha Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Selemani Jafo katika mkutano wa pili wa BRELA na Wadau wake uliofanyika leo Oktoba 25,2024 Jijini Dar es Salaam ukiwa na lengo la kujadili fursa, mafanikio pamoja na changamoto zilizopo na namna Taasisi hii ilivyojipanga kuwahudumia wadau wake siku za mbeleni.
“Matumizi ya mifumo hiyo imepunguza muda, gharama na bughudha kwa Wawekezaji na Wafanyabiashara ambao walikuwa wanasafiri umbali mrefu kufika katika Ofisi za BRELA Dar es Salaam kwa ajili ya kupata huduma hizo”amesema Mhe.Kigahe
Ameongeza kwa kusema kuwa mkutano huu ni muhimu katika kuimarisha ushirikiano kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi ili kuweza kujitathmini katika utoaji wa huduma, kupokea maoni ya wadau na kutoa majibu pamoja na kuchukua yale mapungufu kwa ajili ya kuyafanyia kazi ili kuimarisha ufanisi wa Taasisi katika kuwahudumia wadau wake.
Mhe Kigahe ameeleza kuwa ufanisi wa utendaji kazi wa BRELA ni muhimu katika ujenzi wa uchumi wa nchi yetu kwani ndipo mahala ambapo biashara zinazaliwa na kuanzishwa. BRELA haiwezi kufanikiwa katika kutekeleza majukumu yake ikiwa peke yake, inategema ushirikiano na ukaribu na Sekta za Umma na Sekta Binafsi.
Aidha Mhe.Kigahe amevutiwa na Kauli Mbiu ya Mkutano huo inayosema “Mifumo ya Kitaasisi inayosomana na Uwezeshaji wa Biashara nchini” kwani ina akisi maelekezo ya Serikali ya kwamba ifikapo Mwezi Desemba, 2024 Taasisi kuwa na mifumo inayosoamana.
Na kutoa rai kwa Taasisi zingine za Serikali ambazo hazina utaratibu wa kuwakutanisha wadau wake kuweza kuiga mfano huo mzuri ili kuweza kujipima kwa kupata maoni na mtazamo kutoka kwa wadau badala ya kujifungia na kujitathmini wenyewe maofisini.
Vilevile amesema Serikali imejipambanua kwa uwazi na dhamira ya kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji kwa kuziwezesha Taasisi za Serikali kutoa miongozo, kuzipa rasilimali fedha, rasilimali watu na vitendea kazi ili watimize wajibu wao kwa ufanisi mkubwa na kufikia malengo ya Serikali.
Utoaji wa huduma kwa njia ya mtandao umerahisisha mambo ambapo wafanyabiashara wanaweza kuomba kusajili au kupata Leseni za Biashara zao wakiwa maofisini kwao na wakapata cheti cha Usajili au Leseni pale walipo bila kuhitaji kufika katika ofisi za BRELA.
Awali akimkaribisha naibu Waziri, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri kwa BRELA, Prof. Neema Mori amesema kuwa, Bodi ya Ushauri ya BRELA itaendelea kusimamia na kutoa ushauri wa jinsi ya kuongeza ufanisi, hadi sasa bodi imeweza kufanikisha kuongeza mapato ya BRELA na hatimaye kutoa gawio la shilingi bilioni 18 kwa serikali.
Kwa Upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA Bw.Godfrey Nyaisa amesema mkutano huo umeshirikisha washiriki kutoka Sekta za Umma kwa maana ya Wizara mbalimbali, Taasisi na Mashirika ya Umma, Sekta Binafsi zenye mashirikisho yenye wanachama wengi, Wawekezaji, Wamiliki wa Viwanda, Wafanyabiashara, Wajasiriamali, Wabunifu, Ofisi za Mawakili na wafanyabiashara wadogo kabisa hivyo mchanganyiko huo utaleta majadiliano yenye tija kwa manufaa ya pande zote mbili.