Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni

Tunaipa Uhai wa Kisheria Biashara yako

Habari

WATUMISHI WANAWAKE BRELA WAPONGEZWA KWA UCHAPAKAZI


WATUMISHI WANAWAKE BRELA WAPONGEZWA KWA UCHAPAKAZI
Watumishi wanawake wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), wamepongezwa kwa utendaji kazi mzuri na kutakiwa kuendelea kuzingatia sheria na kanuni za kazi na kuiwezesha Taasisi kufikia malengo yake.

Pongezi hizo zimetolewa tarehe 8 Machi, 2023 na Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA Bw. Godfrey Nyaisa, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku wa Wanawake Duniani, katika ofisi za BRELA jijini Dar es Salaam.

Bw. Nyaisa amewapongeza wanawake wa BRELA kwa kuendelea kutimimza majukumu yao kwa weledi wakati wote.

“Kwanza niwapongeze wanawake wote kwa pamoja pia muongeze bidiii katika kutimiza majukumu yenu ikiwa ni pamoja na kuzingatia Maadili Sheria na Kanuni za kazi” amesema Bw. Nyaisa.

“Wanawake mmekua chachu ya mafanikio makubwa, wengi wenu mnajitoa kwenye shughuli nyingi, mwanamke wa sasa sio kama wa kale, hivyo hongereni kwa kuwa mstari wa mbele kwenye kupambania maisha yenu na
ninawatakia maadhimisho mema na maandamano yenye tija wanawake wote”, amesisitiza Bw. Nyaisa.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Miliki Ubunifu Bi. Loy Mhando, amewapongeza wanawake kwa kujituma na kujitambua kwenye kutimiza majukumu yao ya kila siku.

Aidha Bi. Mhando amewataka Wanawake wa BRELA kutokata tamaa mara wanapokumbana na changamoto zozote.

Wanawake wa BRELA baada ya kupata nasaha hizo walishiriki katika maandamano yaliyoandaliwa kimkoa katika Viwanja vya Mnazi Mmoja na kisha kupeleka mahitaji muhimu kwa wagonjwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kituo cha kulea watoto yatima cha Maunga Center, kilichopo kinondoni, jijini Dar es Salaam.
Maadhimisho ya Siku ya Wanawake huadhimishwa tarehe 8 Machi kila mwaka duniani kote.