Habari
WATUMISHI WA BRELA WAKUMBUSHWA WAJIBU WAO
WATUMISHI WA BRELA WAKUMBUSHWA WAJIBU WAO
Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), imeandaa mafunzo ya siku tano kwa watumishi wake kutoka Kurugenzi ya Kampuni na Majina ya Biashara ili kuwejengea uwezo na kuwaongezea ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Mafunzo hayo yameanza Januari 30, 2023 katika ukumbi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Posta, jijini Dar es salaam, yakienda sambamba na kuwakutanisha na watalaamu kutoka kada nyingine ambao watabadilishana uzoefu.
Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo hayo Kaimu Mkurugenzi wa Kampuni na Majina ya Biashara Bw. Meinrad Rweyemamu amesema kuwa mafunzo hayo yameratibiwa kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kutambua changamoto za wadau wanapo hitaji huduma za BRELA.
"Mafunzo haya ni muhimu katika kuboresha namna ya Utendaji kazi, hivyo ni vyema kila mmoja kuzingatia kuanzia mwanzo mpaka mwisho kwani tutapitia baadhi ya vipengele katika sheria ya Kampuni na kuona vile tunavyovitekeleza na jinsi wadau wanavyotupokea nje, yatakuwa mafunzo yenye majadiliano zaidi. Mkumbuke Msajili ndiye anatunza taarifa za Kampuni zote kwahiyo tutakuwa na mada tofauti ambazo zitawaongezea ujuzi na mfahamu huko nje wanatafsiri vipi sheria hizi", amesema Bw. Rweyemamu
Sambamba na hayo amezitaja faida mbalimbali za kuandaa mafunzo kama hayo ikiwa ni pamoja na kufahamu kipi wateja wa nje wanakumbana nacho na kuona namna ya kuongeza utendaji kwa watumishi wa idara yake na kuzitatua changamoto za wadau kwa wakati.
Akiwasilisha mada kuhusu maswala ya Ufilisi katika Mafunzo hayo, Wakili wa Kujitegemea Bw.Charles Rwechungura amefafanua kwa kina kuhusu sheria ya Makampuni kwa upande wa Ufilisi, na hatua za usajili wa Mikopo.
Amewakumbusha watumishi kuhakikisha wanazingatia kuhakiki nyaraka mbalimbali kwa umakini ambazo zinatakiwa na msajili wakati wa usajili wa mikopo huku akichangia uzoefu wake katika masuala ya ufilisi wa Kampuni na namna ambavyo sheria inataka ili kuhakikisha Kampuni ambazo zimeanzishwa zinakidhi matakwa yake.
Msajili ni mtekelezaji wa Sheria ya Makampuni Sura 212, hivyo elimu hii itawasadia kuongeza uelewa na namna taratibu za ufilisi/uokozi wa Kampuni zinafanyika kabla nyaraka zake kuwasilishwa kwa msajili pia imewaongezea maarifa ya namna ya kuwashauri wateja kwenye masuala yahusuyo Kampuni.
Mafunzo hayo ya siku tano yatahitimishwa rasmi tarehe 3 Februari, 2023.