Habari
WATUMISHI BRELA WAPIGWA MSASA JUU YA TEHAMA NA SHERIA
WATUMISHI BRELA WAPIGWA MSASA JUU YA TEHAMA NA SHERIA
Watumishi wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), wamepatiwa elimu kuhusu programu za Kompyuta (Software) inavyoweza kulindwa kisheria katika Hataza (Patent).
Akitoa elimu hiyo katika mafunzo yanayoendelea kwenye Ukumbi wa Chuo cha Utumishi wa Umma jijini Dar es Salaam, Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma Mhe. Dkt. Adam Mambi ameelezea kuhusu vigezo,utaratibu wa kutambua na kusajili programu za kompyuta (Software) kama Hataza (Patent).
Jaji Mambi amezungumzia pia kuhusu Sheria na Mikataba ya Kimataifa inayolinda Ubunifu katika programu za kompyuta (Software protection) ambayo itawezesha kurahisisha utoaji wa Hataza kwa waombaji.
“Tukatumie mafunzo haya kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zinazoongoza utumishi wetu na mkatoe elimu hii kwa watumishi wengine kila fursa ya kufanya hivyo inapopatikana”, amesisitiza Jaji Mambi.
Amefafanua kuwa elimu hiyo itasaidia kujua namna ya kulinda haki za watu wanaobuni mifumo mbalimbali ya kompyuta na Teknolojia.
Aidha, Dkt. Mambi amesema mafunzo hayo yatasaidia kujua faida za kusajili majina ya biashara na kampuni kupitia mtandao, vilevile kujua sheria zinazosimamia matumizi ya huduma za kimtandao na usalama wa kimtandao (Cyber-Laws).
“Washiriki wa mafunzo mkiwa kama wasaidizi wa Msajili katika utoaji wa huduma na Miliki-bunifu, mafunzo haya yatawasaidia kujua njia za kiusalama mtandaoni kama vile matumizi ya saini za kieletroniki (Digital Signatures)na nywila (Password)," amefafanua Jaji Mambi.
Mh.Dr Mambi pia aliwafundisha washiriki juu namna ya kutambua haki na kulinda Alama za Biashara (Trade&Service Marks) pamoja namna migogoro inavyoweza kutokea kati ya Alama za Biashara (Trademarks)na Majina ya Utambuzi mitandaoni (Domain names)
Aidha, Dkt. Mambi amesema mafunzo hayo yatasaidia kutatua changamoto za TEHAMA katika eneo Miliki Ubunifu (Intellectual Property) ikiwa ni pamoja na uelewa wa sheria.
Mafunzo hayo ya siku mbili yamehitimishwa rasmi leo tarehe 10 Februari, 2023.