Habari
WATAALAM WA UNUNUZI NA UGAVI WASHAURIWA KUITUMIA BRELA KWENYE MAJUKUMU YAO
WATAALAM WA UNUNUZI NA UGAVI WASHAURIWA KUITUMIA BRELA KWENYE MAJUKUMU YAO
Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi wameshauriwa kuitumia Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), wanapotekeleza majukumu yao ili kuepusha kuvunja sheria, kanuni na taratibu za Ununuzi.
Kauli hiyo imetolewa leo tarehe 7 Desemba, 2022 na Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Bw. Godfrey Nyaisa, kwenye Kongamano la 13 la Ununuzi na Ugavi katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa(AICC), Jijini Arusha.
"Wataalam mnapofanya tathmini za zabuni msitegemee tu cheti cha usajili wa kampuni bali muwasilishe maombi kwa Msajili ili awape taarifa za kina juu ya uhai wa kampuni zinazoomba zabuni", amesisitiza Bw. Nyaisa
Bw. Nyaisa amefafanua kuwa wanapoitumia BRELA kupata taarifa, itawasaidia kuepusha hoja za kikaguzi na watafanya kazi kwa weledi na uwazi kwakuwa watapata taarifa za kina za umiliki halali wa kampuni, wanahisa wa kampuni na uhai wa kampuni inayoomba Zabuni.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Makampuni na Majina ya Biashara kutoka BRELA, Bw. Meinrad Rweyemamu, katika wasilisho lake mbele ya watalaamu hao amewaeleza kuwa BRELA ina majukumu mengi baada ya kusajili Kampuni na majukumu hayo ni vizuri wataalam wa ununuzi na ugavi kuyafahamu na kuyatumia kwenye utekelezaji wa majukumu yao.
Akifafanua kauli hiyo, Bw. Rweyemamu amesema kuwa baadhi ya wataalamu wa ununuzi wanaingia mikataba na kampuni ambazo haziwasilishi taarifa za mwaka na hatari yake ni kuwa taasisi husika inaingia makubaliano na kampuni ambayo haina uhai.
Bw. Rweyemamu amesema kuwa kampuni zinapowasilisha taarifa ya mwaka inamjulisha Msajili pia endapo kuna mabadiliko yoyote katika Kampuni na taratibu za mabadiliko hayo zimezingatiwa.
Wakati huohuo Mkurugenzi wa Ununuzi na Ugavi kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Boaz Ibrahim, ameishukuru BRELA kwa kutoa elimu hiyo kwa wataalam hao ili kuepusha kutokufanya kazi kwa maadili na kuziingizia taasisi zao hasara.
BRELA inashiriki kongamano la 13 la Ununuzi na Ugavi linaloendelea hadi tarehe 8 Desemba, 2022 na inatoa huduma mbalimbali za Sajili.