Habari
WAHARIRI WATAKIWA KUWA MABALOZI WA BRELA KWA WANANCHI
WAHARIRI WATAKIWA KUWA MABALOZI WA BRELA KWA WANANCHI
Wahariri wa Vyombo vya habari nchini, wametakiwa kuwa mabalozi wazuri kwa Wananchi kuhusu dhana ya Umiliki Manufaa katika Kampuni kwa kuwapa taarifa sahihi kupitia vyombo vya habari ambavyo wanavitegemea.
Hayo yamebainishwa leo tarehe 8 Juni, 2023 na Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania, Bw. Deodatus Balile katika Warsha ya Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) na wahariri hao iliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC).
Bw. Balile ambaye alikuwa Mgeni Rasmi katika Warsha hiyo ameeleza kuwa zoezi hilo linafanyika mahususi kwa ajili ya kupeana uzoefu na uelewa wa pamoja ili kuifikishia jamii taarifa sahihi.
“Baada ya Warsha hii, ni imani yangu kwamba mtakuwa mmepata uelewa wa kutosha ambao utawasaidia kuwakumbusha Watanzania juu ya muda, taratibu na umuhimu wa uwasilishaji wa taarifa za Wamiliki Manufaa katika Kampuni kwa mujibu wa sheria”, amesema Bw. Balile.
Awali akitoa hotuba ya ukaribisho kwa niaba ya Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Mkurugenzi wa Leseni, Bw. Andrew Mkapa ameeleza kuwa Wakala inatambua kuwa wahariri ni kiungo muhimu katika kuhamasisha urasimishaji biashara nchini.
“BRELA inatambua mchango wa Wahariri kwenye utekelezaji wa shughuli zake na kwa sababu hiyo imekuwa ikiwashirikisha kuhusu marekebisho na maboresho mbalimbali yanayofanyika au yanayoendelea kisheria na kimfumo lengo ni kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi wakati wote”, amesema Bw. Mkapa.
Uwasilishaji wa taarifa za Miliki Manufaa unatokana na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitisha marekebisho ya Sheria ya Kampuni, Sura 212 kwa lengo la kuwezesha upatikanaji wa taarifa za Kampuni zilizosajiliwa na zinazoendelea kusajiliwa.
Mwaka 2022, Kanuni za Umiliki Manufaa katika Kampuni zilipitishwa na kuanza kutumika rasmi, malengo makuu yakiwa ni kuboresha mazingira rafiki ya uwekezaji, kuzuia ukwepaji kodi pamoja na kudhibiti utakatishaji fedha haramu na ufadhili wa vitendo vya kigaidi.