Habari
WAFANYABIASHARA WASISITIZWA KUINGIZA BIDHAA SOKONI BAADA YA KUSAJILI ALAMA BRELA
WAFANYABIASHARA WASISITIZWA KUINGIZA BIDHAA SOKONI BAADA YA KUSAJILI ALAMA BRELA
Wafanyabiashara wanaozalisha bidhaa na kutoa huduma katika Wilaya ya Nyamagana Jijini Mwanza wamesisitizwa kuingiza bidhaa wanazozizalosha na huduma wanazozitoa sokoni, baada ya kuzisajili Alama za Biashara na Huduma hizo kwa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) ili kujipatia ulinzi wa kisheria na kuhimili ushindani katika soko.
Wito huo umetolewa leo tarehe 13 Novemba, 2023 na Kaimu Mkuu wa Sehemu ya Hataza kutoka BRELA, Bi. Neema Kitala wakati wa mafunzo kwa wafanyabaishara wanaozalisha bidhaa na kutoa huduma mbalimbali kutoka Wilaya ya Nyamagana na kufanyika katika ukumbi wa mikutano wa Nyakahoja Jijini Mwanza.
“Uzuri wa kusajili Alama ya Biashara na Huduma yako ni kukitambulisha kile unachokizalisha sokoni na faida kubwa utakayoipata ni bidhaa yako kutambulika na kuaminika katika masoko, bidhaa hiyo kuonekana halali na ya kipekee, pia inakupa faida ya kupenya katika masoko mbalimbali ndani na nje ya nchi,” amesisitiza Bi. Kitala.
Aidha, Bi. Kitala amefafanua kuwa, wafanyabiashara wasiposajili Alama za Biashara na Huduma zao, pindi wanapotambulisha biashara zao sokoni, licha ya kupendwa na watumiaji, hazitakuwa na ulinzi wa kisheria, hivyo mtu mwingine anaweza akaiga, akasajili na kuingiza sokoni hivyo kusababisha migogoro ambapo utatuzi wake hutumia muda na gharama kubwa.
Naye mfanyabiashara wa chakula cha mifugo Wilayani humo, Bi. Wilhelmina Kubingwa, amesema, mafunzo hayo yatamuwezesha kusajili Alama ya Biashara anayotumia katika bidhaa zake, hivyo ili kuweza kushindana katika soko ni muhimu kuweka ulinzi wa bidhaa zake kwa kusajili Alama anayotumia.
Wakati huohuo, Afisa Sheria kutoka BRELA, Bw. Calvin Rwambongo, ameongeza kwa kusema kuwa, BRELA inasimamia Sheria za Miliki Ubunifu ambazo ni Sheria ya Alama za Biashara na Huduma na Sheria ya Hataza.
Bw. Rwambongo amesema kuwa Sheria ya Alama ya Biashara inalenga kuwalinda wazalishaji wa bidhaa na huduma wanaobuni alama, nembo, michoro, ishara mbalimbali kwa lengo la kutofautisha bidhaa zao wanapoingiza sokoni na Sheria ya Hataza ni haki ya kipekee ya ulinzi inayompa mbunifu wa bidhaa mpya au mchakato mpya unaolenga kutatua changamoto za kiufundi.
Ameongeza kuwa, Sheria ya Alama za Biashara na Huduma iko wazi kwamba Alama inaposajiliwa inazuia wengine kutumia Alama huaika pasipo idhini ya yule aliyesajili hivyo inamtambua kwa kumpa ulinzi yule tu aliyesajili na itampa haki yake endapo mtu mwingine atatumia Alama kama hiyo na kuiingiza sokoni.
Aidha, Rwambongo amewashauri wazalishaji wa biashara na huduma kukimbilia BRELA kulinda haki zao na kutotumia Alama za Biashara na Huduma za watu wengine kwakuwa athari yake ni kubwa ambayo inaweza kusababisha bidhaa zake kuteketezwa na kulipa fidia.
BRELA inatoa mafunzo kwa Wafanyabiashara kuhusu usajili wa Alama za Biashara na Huduma kuanzia tarehe 13 hadi Novemba hadi 17 Novemba, 2023 katika Wilaya za Nyamagana, Ilemela, Misungwi na Ukewe