Habari
WAFANYABIASHARA SIRARI WATAKIWA KUWA MABALOZI WA HUDUMA ZA BRELA
WAFANYABIASHARA SIRARI WATAKIWA KUWA MABALOZI WA HUDUMA ZA BRELA
Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Kanali Michael Mtenjele amewataka wafanyabiashara katika kata ya Sirari wilayani humo, kuwa mabalozi wa huduma za urasimishaji wa biashara zinazotolewa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA).
Rai hiyo imetolewa Februari 20, 2023 katika kata hiyo wakati wa ufunguzi zoezi la uelimishaji umma kwa wafanyabiashara wa madini, mazao, mifugo, na wamiliki wa Viwanda vikubwa na vidogo kwenye ukumbi wa Mongo, Sokoni wilayani Tarime.
Akizungumza katika hotuba yake ya ufunguzi, Kanali Mtenjele ameeleza kuwa mafunzo hayo yana lengo la kuhakikisha kuwa huduma zinazotolewa na BRELA zinawafikia wananchi kwa karibu zaidi na kuwapunguzia kero pamoja na gharama zisizokuwa za lazima katika urasimishaji wa biashara hapa nchini.
“Wafanyabiashara ni vyema kutambua kuwa unaporasimisha biashara yako unashiriki katika kuchangia pato la Taifa ambalo hatma yake ndio linaiwezesha Serikali kutoa huduma mbalimbali za kijamii kwa wananchi wote.
Lakini pia mnapata fursa ya ya kuimarisha biashara zenu na kujiweka katika nafasi nzuri hasa katika zama hizi za ushindani wa kibiashara ikiwemo uwezekano wa kupata fursa mbalimbali zinazotolewa ama na Serikali au Taasisi mbalimbali za kifedha”, ameeleza Kanali Mtenjele.
Kwa upande wake Mkuu wa Msafara kutoka BRELA Bi. Beatrice Masele amewapongeza wafanyabiashara wa kwa kuacha shughuli zao na kufika katika zoezi hilo ili kupata elimu pamoja na huduma za papo kwa papo.
“Ni matarajio yangu kwamba, baada ya kupata elimu hii, wafanyabiashara mtasajili Majina ya Biashara, Makampuni, Alama za Biashara na Huduma , wenye viwanda vidogo, msajili ili kupata vyeti vya usajili, na wenye viwanda vikubwa mpate leseni ya viwanda na kufanya biashara na kutimiza matakwa ya kisheria”, amesema Bi. Masele.
Zoezi hilo la uhamasishaji kwa umma limeanza kutekelezwa kuanzia tarehe 20 na 21 Februari, 2023 Sirari, Tarime mkoani Mara. Zoezi hili litaendelea katika Wilaya ya Bariadi, Simiyu tarehe 23, 24 na 25 Februari, 2023 na kisha litahitimishwa Kahama, Shinyanga tarehe 27 Februari hadi tarehe 1 Machi, 2023.