Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni

Tunaipa Uhai wa Kisheria Biashara yako

Habari

WADAU WAKUTANA KUTOA MAONI YA MAREKEBISHO YA SHERIA YA LESENI ZA BIASHARA


Wadau wa biashara kutoka Taasisi za Serikali na Sekta Binafsi wanakutana kwa siku tatu na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), kutoa maoni juu ya marekebisho ya Sheria ya Leseni za Biashara Sura 208.

Hatua hiyo inafuatia mpango wa Serikali wa kuifanyia marekebisho Sheria ya Leseni za Biashara Sura 208 ili iendane na hali ya sasa, baada ya kubainika kuwa Sheria hiyo imepitwa na wakati.

Hayo yameelezwa leo tarehe 14 Septemba, 2022 Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Leseni kutoka BRELA, Bw. Andrew Mkapa wakati wa kikao cha kukusanya maoni ya wadau kuhusu marekebisho ya Sheria ya Leseni za Biashara Sura 208.

Bw. Mkapa amesema Sheria ya Leseni za Biashara kama ilivyo kwa sheria nyingine za nchi, haitakiwi kuwa mgando na zinatakiwa kwenda na wakati, hivyo Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, kupitia BRELA imeona ni vema kuifanyia marekebisho sheria hiyo.

Bw. Mkapa ambaye amefungua kikao hicho kwa niaba ya Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA amesema, hivi sasa limeibuka suala la biashara za mitandaoni ambalo nalo linatakiwa kuangaliwa kisheria ili kwenda sambamba na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

"Hatua iliyopo sasa ni ya kikosi kazi kuchukua maoni na kuyapeleka serikalini kwa ajili ya kufanyiwa marekebisho kwa sheria hiyo", amefafanua Bw. Mkapa.