Habari
WADAU WAHIMIZWA KUWASILISHA TAARIFA ZA WAMILIKI MANUFAA
WADAU WAHIMIZWA KUWASILISHA TAARIFA ZA WAMILIKI MANUFAA
Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), imewahimiza wadau wake kuwasilisha taarifa za Wamiliki Manufaa kwa wakati ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza.
Wito huo umetolewa leo Februari 06, 2024 katika warsha iliyowakutanisha wadau ikiwa ni pamoja na wamiliki wa kampuni katika ukumbi wa hoteli ya Victoria Palace Jijini Mwanza.
Akizungumza katika warsha hiyo Afisa Mwandamizi Kutoka BRELA Bw. Meinrad Rweyemamu amesema ni wajibu wa kila mmiliki wa kampuni kukumbuka kuwasilisha taarifa za Wamiliki Manufaa kwa Msajili wa Kampuni kama inavyotakiwa kisheria.
Ameongeza kuwa mbali na umuhimu wake katika masuala ya kiusalama pia zinasaidia kwenye uwajibikaji na uwazi katika uendeshaji wa kampuni.
"Tupo hapa kuwakumbusha kuhusu dhana ya Miliki Manufaa ambapo kila anayemiliki zaidi ya asilimia tano ya hisa za kampuni na anashiriki kufanya maamuzi moja kwa moja au kupitia mtu mwingine ndiyo walengwa hasa ambao taarifa zao zinapaswa kuwalishwa BRELA kila mwaka," amesema Bw. Rweyemamu.
Ameongeza kuwa pale wanapowasilisha taarifa hizo kwa wakati huepuka adhabu inayotokana na ucheleweshaji wa taarifa hizo.
Awali akizungumza katika ufunguzi wa warsha hiyo, mwakilishi wa Katibu Tawala wa mkoa wa Mwanza Bw. Daniel Machunda, ameipongeza BRELA kwa jitihada mbalimbali inazozifanya ikiwa ni pamoja na kuandaa warsha na mafunzo ambayo yanalenga kuwakumbusha wadau wajibu wao baada ya kukamilisha sajili mbalimbali BRELA.
Pia ametoa wito kwa wafanyabiashara na wajasiriamali katika jiji la Mwanza kutumia fursa hiyo na kuwataka wafike pale wanapohitajika ili kupata msaada wa haraka na kuepuka kutumia watu kati ambao hawatimizi wajibu kwa haraka.
Pia amewataka wenye changamoto mbalimbali na wa wenye uhitaji wa huduma za BRELA kufika katika viwanja vya Rock City Mall kuanzia Tarehe 7 hadi 9 Februari, 2024 ili kupata huduma za papo kwa papo.
BRELA imekuwa ikifanya warsha na kliniki mbalimbali katika mikoa ya Arusha, Dodoma, Mbeya, Dar es salaam, kuhamasisha wadau mbalimbali kuhusu umuhimu wa kuwasilisha taarifa za Wamiliki Manufaa.