Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni

Tunaipa Uhai wa Kisheria Biashara yako

Habari

ULINZI WA MILIKI UBUNIFU KATIKA RASILIMALI ZA KIJENETIKI NA UJUZI WA JADI KUNUFAISHA NCHI NA JAMII ZA KIJADI


 

ULINZI WA MILIKI UBUNIFU KATIKA RASILIMALI ZA KIJENETIKI NA UJUZI WA JADI KUNUFAISHA NCHI NA JAMII ZA KIJADI

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) imeandaa kikao cha mashauriano na Wadau kuhusu Sheria ya Kimataifa ya Shirika la Miliki Ubunifu (World Intellectual Property - WIPO) itakayolinda Miliki Ubunifu katika Rasilimali za Kijenetiki na Ujuzi wa Jadi kilichofanyika tarehe 23 Februari, 2024 Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho, Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA Bw. Godfrey Nyaisa amesema kuwa mashauriano hayo yanalenga kujadili na kuona namna bora Nchi itakavyoweza kunufaika na Sheria hiyo ya Kimataifa ambayo ikikamilika italeta manufaa kwa Nchi na Jamii za Kijadi kupitia Miliki Ubunifu zitakazotokana na Rasilimali hizo.

Amesema kuwa katika Ulimwenguni huu wa Sayansi na Teknolojia ni vyema bunifu zinazotokana na Rasilimali za Kijenetiki na Ujuzi wa Jadi zikawaletea manufaa wamiliki hasa jamii ambazo rasilimali na ujuzi huo unapatikana. Hivyo Sheria ya Kimataifa kuhusu Ulinzi wa Rasiliamli hizo imekuja kwa muda muafaka ili kuzuia matumizi yasiyo halali ya Rasilimali hizo kwa kuweka uwazi na kuwaletea faida wahusika.

Ameongeza kuwa, tiba za jadi au mbadala zimesaidia katika kutoa kinga na tiba kwa magonjwa mengi hapa nchini ambapo toka enzi jamii zimekuwa zikitumia tiba hizo, hii inathibitishwa na Ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ya 2019 ambayo inabainisha kuwa zaidi ya asilimia 79 ya watanzania wanatumia tiba za jadi.

"Tunatambua kuwa Taifa letu limejaliwa kuwa na rasilimali nyingi za kijenetiki zitokanazo na Mimea, wanyama na ujuzi wa jadi ambavyo vina thamani ambayo wengi hawafahamu na mara nyingine rasilimali hizo kutumiwa na watu wengine pasipo kuwaletea manufaa wahusika. Kwa sasa tumejipanga kusaidia wabunifu waweze kulinda bunifu zao na baada ya ulinzi wafaidike na bunifu hizo, na matumizi ya rasilimali hizi yawe na faida kwa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla" amedokeza Bw. Nyaisa.

Amepambanua kuwa Jamii yetu imekuwa na watafiti mbalimbali na wataalamu ambao hubuni vitu mbalimbali ikiwepo dawa za jadi ambazo zikilindwa na kutumika ipasavyo zinaweza kuwapatia wamiliki wa bunifu hizo manufaa makubwa.

Akitoa wasilisho kuhusu Sheria ya Kimataifa ya WIPO juu ya Miliki Ubunifu katika Rasilimali za Kijenetiki na Ujuzi wa Jadi, Kaimu Mkurugenzi wa Milki Ubunifu kutoka BRELA Bi. Loy Mhando amesema kuwa kupitia Sheria hiyo nchi wanachama za WIPO ikiwemo Tanzania, zitafaidika na bunifu zitokanazo na Rasilimali za Kijenetiki na Ujuzi wa Jadi kutoka katika Nchi hizo. Sheria hii itazuia matmizi ya rasilimali hizo pasipo kufichua mahali zinapopatikana na kuhakikisha jamii husika zinapata faida itokanayo na matumizi ya rasilimali hizo. watalindwa na kupewa haki ya kipekee katika matumizi ya Rasilimali hizo.

Kwa kuhutimisha amesema kuwa majadiliano ya Sheria hiyo yatazaa Itifaki ambayo itakamishwa Mwezi Mei 2024 katika mkutano wa kidplomasia utakaofanyika makao makuu ya WIPO Jijini Geneva, Uswisi.