Habari
TANZANIA YASAINI MKATABA WA KIHISTORIA WA KIMATAIFA WA WIPO
TANZANIA YASAINI MKATABA WA KIHISTORIA WA KIMATAIFA WA WIPO
Dar es Salaam-26 Mei, 2024
Tanzania yaungana na nchi wanachama wa Shirika la Miliki Ubunifu Duniani (WIPO) kupitisha
na kusaini Mkataba wa kihistoria wa kimataifa kuhusu Miliki Ubunifu, Rasilimali za Kijenetiki na
Maarifa ya Jadi.
Mkataba huo unalenga kulinda haki za wenyeji asilia na jamii za kijadi katika kuhakikisha
matumizi ya rasilimali za kijenetiki na maarifa ya jadi katika tafiti na vumbuzi yanaleta faida kwa
jamii hizo.
Mkataba huo wa kihistoria na wa aina yake umejadiliwa kwa takribani miaka 25 na nchi
wanachama wa WIPO kabla ya kupitishwa rasmi tarehe 24 Mei, 2024 katika Mkutano wa
Kidiplomasia uliofanyika katika Makao Makuu ya Shirika hilo Jijini Geneva, Uswisi.
Mheshimiwa Dkt. Abdallah S. Possi, Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika
Umoja wa Mataifa na Mashirika ya Kimataifa Jijini Geneva aliongoza ujumbe wa Tanzania
katika Mkutano huo wa Kidiplomasia uliopitisha Mkataba tajwa, na kusaini Mkataba kwa upande
wa Tanzania.
Walioshuhudia hafla ya utiaji saini mkataba huo ni Bw. Godfrey Nyaisa, Afisa Mtendaji wa
BRELA, Bw. Twalib Njohole, Msajili wa Hakimiliki za Wagunduzi wa Aina Mpya za Mbegu za
Mimea kutoka Wizara ya Kilimo, Bi. Loy Mhando, Mkurugenzi wa Miliki Ubunifu kutoka BRELA
na Bi. Zulekha Fundi, Afisa Mambo ya Nje kutoka Ubalozi wa Tanzania Geneva.
Baada ya Mkataba huu kuridhiwa na nchi, Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA)
na Wakala wa Usajili wa Biashara na Mali (BPRA) watakuwa na jukumu la kuhakikisha
waombaji wa ulinzi wa Vumbuzi kupitia Sheria za Hataza wanafichua taarifa za mahali
zilipopatikana rasilimali za kijenetiki na maarifa ya jadi yaliyotumika katika tafiti na vumbuzi
husika.
Vilevile, kufuatilia matumizi ya rasilimali hizo zinazopatikana hapa nchi ambazo watafiti na
wavumbuzi kutoka nchi nyingine wanazitumia katika tafiti na vumbuzi zao ili kuhakikisha
wamiliki wa rasilimali hizo hapa nchini wanapata faida zitakazotokana na matumizi ya rasilimali
hizo.
Mkataba huu utaanza kutumika rasmi siku 30 baada ya nchi 15 kuwasilisha nyaraka za
uridhiwaji wa Mkataba huo katika Ofisi za WIPO.