Habari
SERIKALI YADHAMIRIA KUBORESHA MAZINGIRA YA BIASHARA
SERIKALI YADHAMIRIA KUBORESHA MAZINGIRA YA BIASHARA
Serikali ya awamu ya Sita imedhamiria kuboresha na kuimarisha mazingira ya biashara nchini ili kuendana na azma ya kufanya mageuzi ya kiuchumi na viwanda kwa ajili ya kuleta maendeleo endelevu ya jamii.
Hayo yamebainishwa leo tarehe 6 Aprili 2024 na Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Ashatu Kijaji wakati akifungua kikao cha Wizara na Wakuu wa Idara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji wa Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kilichofanyika mkoani Morogoro.
Dkt. Kijaji amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa jitihada zake ni kutengeneza mahusiano mazuri na Wafanyabiashara ili kukuza uchimi wa Taifa.
“Dunia imeshaingia katika mapinduzi ya Nne ya Viwanda ambayo yanajikita katika matumizi makubwa ya teknolojia na uharaka wa utoaji wa huduma, watu kukutana kidigitali na uwepo wa maarifa ya pkutosha na yasiyo na mipaka kwa jamii ili kuongeza uzalishaji wa bidhaa na huduma kwa njia za kidigitali”, amesisitiza Dkt. Kijaji.
Aidha, Dkt. Ashatu Kijaji amewataka Wizara na Maafisa Biashara wa Mikoa na Wakuu wa Idara za Biashara, Viwanda na Uwekezaji kukaa pamoja na kujadili mustakabali wa kukumbushana wajibu 0wa kutekeleza Sera, Sheria, Kanuni pamoja na taratibu zinazohusu biashara na viwanda katika Halmashauri zao.
“Nimewaiteni ninyi nikitambua kwamba ndiyo mlioaminiwa kuongoza sehemu na Idara za Viwanda Biashara na Uwekezaji katika Mamlaka zenu ili tuyatafsiri na kuyaelewa kwa pamoja majukumu mliyonayo, matarajio na matokeo tarajiwa ya uanzishwaji wa Sehemu na Idara hizo katika maeneo yenu”, amesema Dkt. Kijaji.
Naye Katibu Mkuu Ofisi ya Raisi Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa -TAMISEMI Ndg. Adolph Ndunguru amesema kuwa mpango wa maendeleo wa serikali ni kuifikisha nchi katika uchumi shindani na kuboresha masoko ya bidhaa zinazozalishwa nchini.
“Kuhakikisha tunachokizalisha kinauzwa, lakini pia kuongeza tija katika uwekezaji ili mpango wetu wa kutengeneza uchumi shindani ufanikiwe kwa kiwango kikubwa” amesema Ndg. Ndunguru
Awali akitoa neno la utangulizi, Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Bw. Godfrey Nyaisa amewapongeza Wakuu wa Idara za Viwanda, Biashara na Uwekezaji kutoka Mamlaka za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa kushiriki katika mkutano huo.
“Kikao kazi hiki kina lengo la kuwajengea uelewa Wakuu wa Sehemu na Idara za Viwanda, Biashara na Uwekezaji kutoka katika Mamlaka za Mikoa na Serikali za Mitaa kuhusu Sheria, Kanuni na Taratibu za sajili na utoaji wa Leseni zinazosimamiwa na BRELA na namna ambavyo tunaweza shirikiana katika kutekeleza majukumu ya kukuza sekta ya biashara na uwekezaji nchini” , amesema Bw. Nyaisa
Kikao kazi hiki kimehudhuriwa na Wakuu wa Sehemu na Idara za Viwanda Biashara na Uwekezaji katika Sekretarieti za mikoa na Mamlaka za Serikali za mtaa wapatao 200, wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara na Wakurugenzi kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI na kinatarajiwa kuhitimishwa tarehe 7 Aprili, 2024 mkoani Morogoro.