Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni

Tunaipa Uhai wa Kisheria Biashara yako

Habari

SERA YA TAIFA YA MILIKI UBUNIFU KUONGEZA MAENEO MAPYA YA ULINZI WA MILIKI UBUNIFU


SERA YA TAIFA YA MILIKI UBUNIFU KUONGEZA MAENEO MAPYA YA ULINZI WA MILIKI UBUNIFU

Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara ipo katika hatua za mwisho za maandalizi ya Sera ya Taifa ya Miliki Ubunifu (National Intellectual Property Policy)

Kauli hii imetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdallah aliyemwakilisha Mheshimiwa Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara katika Maadhimisho ya siku ya Miliki Ubunifu yaliyoandaliwa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) na kufanyika tarehe 28 Aprili, 2023 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.

Dkt. Abdallah amesema kuwa kukamilika kwa Sera hii kutasaidia kutoa miongozo itakayoimarisha miundo ya kisheria na kitaasisi katika kusimamia masuala ya Miliki Ubunifu, kuwa na taratibu rahisi na wezeshi za sajili na linzi mbalimbali, kuimarisha linzi zaidi na kuongeza maeneo mapya ya ulinzi wa Miliki Ubunifu.

"Serikali chini ya uongozi mahiri wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali hususan utekelezaji wa malengo ya Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara (Blueprint), ili kuweka mazingira bora na wezeshi katika sekta zote ikiwa ni pamoja na eneo la Miliki Ubunifu ambalo linakuwa kwa kasi duniani", amesisitiza Dkt. Abdallah

Ameongeza kuwa Serikali imeanza mchakato wa kufanya mapitio ya Sheria mbalimbali za Miliki Ubunifu kwa kuwa baadhi ya Sheria hizo zimepitwa na wakati na baadhi ya maeneo hayalindwi kisheria, hivyo itakapokamilika usimamizi wa masuala ya Miliki Ubunifu utakuwa rafiki na wezeshi kwa wafanyabiashara kwa ajili ya kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa ujumla.

Kwa upande wake, Mjumbe wa Bodi ya Ushauri ya BRELA, Bi. Judith Kadege, ambaye alimuwakilisha Mwenyekiti wa Bodi hiyo, amesema kuwa mfumo wa usajili wa ulinzi wa Miliki Ubunifu Tanzania utasaidia kuweka ulinzi katika ubunifu unaofanywa na wafanyabiashara na wabunifu mbalimbali hasa katika kipindi ambacho teknolojia inaendelea kukua kwa kasi.

Awali akizungumza katika maadhimisho hayo, Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA Bw. Godfrey Nyaisa, amesema kuwa Taasisi itaendelea kuboresha mifumo yake ya ndani ya sajili na kuweka mikakati mizuri ya kuboresha huduma wanazotoa na kuvutia zaidi wabunifu wa kazi mbalimbali ili kuongeza idadi ya sajili na linzi za kazi zao pamoja na kuhakikisha wabunifu hao wanapata manufaa ya kazi hizo. Mikakati hiyo ni pamoja na uanzishaji wa maadhimisho hayo, mashindano na Tuzo za Miliki Ubunifu nchini ambayo yanategemewa kuanza hivi karibuni, kushirikiana na kutembelea wadau wa Miliki Ubunifu kama vile Taasisi na Vyuo pamoja na shule ili kutoa elimu ya Hataza na masuala mengine ya Miliki Ubunifu.

Bw. Nyaisa amesema lengo ni kuhakikisha kuwa Miliki Ubunifu inatumika kama chachu ya ukuaji wa uchumi wa mtu binafsi na Taifa kwa ujumla kutokana na umuhimu wake katika maendeleo.

Kwa mwaka 2023 maadhimisho ya Miliki Ubunifu yamebeba kauli mbiu isemayo "Wanawake na Miliki Ubunifu: Kuongeza kasi ya Ubunifu katika Biashar