Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni

Tunaipa Uhai wa Kisheria Biashara yako

Habari

RC KIGOMA ARIDHISHWA NA UTENDAJI WA BRELA


RC KIGOMA ARIDHISHWA NA UTENDAJI WA BRELA

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe. Thobias Andengenye ameipongeza Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), kwa jitihada inazozifanya za kuwezesha wananchi kurasimisha biashara zao na namna inavyotoa huduma katika Maonesho ya sita (6) ya Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC).

Pongezi hizo amezitoa leo tarehe 27 Mei, 2023 alipotembelea banda la BRELA kabla ya kufunga maonesho hayo ambayo yamefanyika katika uwanja wa Mwanga, Mjini Kigoma.

Mhe. Andengenye amesema ameridhishwa na namna BRELA inavyotekeleza majukumu yake, wakati akipatiwa maelezo na Afisa Usajili wa BRELA Bw. Stanslaus Kigosi, juu ya ushiriki wa BRELA katika maonesho hayo.

Akitoa maelezo hayo kwa Mkuu wa mkoa, Bw. Kigosi, ameeleza kuwa katika maonesho hayo mbali na kutoa elimu pia wamekua wakitoa usaidizi kwa wadau mbalimbali kwenye Mfumo wa Usajili kwa njia ya Mtandao, pamoja na kutoa huduma za usajii za papo kwa papo.

“Huduma zote za BRELA zinazotolewa kwa njia ya mtandao, hivyo baadhi ya wananchi wamekuwa wakipata changamoto katika kupata huduma hizo, uwepo wetu hapa ni kuwawezesha kupata huduma hizo zikiwemo Usajili wa Majina ya Biashara, Usajili wa Makampuni na Utoaji wa Leseni za Biashara Kundi "A" papo kwa papo”, amesema Bw. Kigosi.

Aidha Bw. Kigosi amezitaja huduma zingine zinazotolewa na BRELA kuwa ni pamoja na Usajili wa Alama za Biashara na Huduma, Utoaji wa Hataza, Utoaji wa Leseni za Viwanda na huduma baada ya usajili.

Katika maonesho hayo pia maafisa wa BRELA wamepata fursa ya kutembelea mabanda ya washiriki wengine na kuwahamasisha kurasimisha biashara zao.

Maonesho hayo ya siku saba yalianza tarehe 21, Mei, 2023 na yamehitimishwa leo tarehe 27 Mei, 2023.