Habari
MWENYEKITI BODI YA USHAURI BRELA APOKEA MAONI YA WAFANYABIASHARA
MWENYEKITI BODI YA USHAURI BRELA APOKEA MAONI YA WAFANYABIASHARA
Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Prof. Neema Mori amepokea maoni kutoka kwa wafanyabiashara waliopata huduma katika mabanda ya BRELA katika maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa yanayoendelea katika uwanja wa Maonesho wa Mwalimu J.K Nyerere, uliopo barabara ya Kilwa, jijini Dar es Salaam.
Maoni hayo ameyapokea leo tarehe 5 Julai, 2023 alipotembelea mabanda ya BRELA na kujionea jinsi watumishi wa BRELA wanavyotoa huduma za sajili, utoaji wa leseni pamoja na elimu kuhusu umuhimu wa urasimishaji biashara.
“Nilifika na kukuta wateja wamekaa na nikapata fursa ya kuongea nao huku wakiwa wanapatiwa huduma, kikubwa nilichojifunza ni kuwa wafanyabiashara hao wamefurahia huduma walizopata maana kwa muda mrefu baadhi ya wateja wamekuwa wakisumbuliwa na watu wa kati lakini walipofika katika mabanda wamepata huduma ndani ya muda mfupi”, amesema Prof. Mori.
Pia, ametoa ushauri kwa wafanyabishara kutambua kuwa Tanzania ni mahali sahihi kwa biashara, hivyo kuwataka kusajili biashara zao BRELA ambao ni lango kuu la biashara na ili kufanya biashara na kufanikiwa amewasihi kufika katika mabanda ya BRELA, kupata ushauri, kuelekezwa, kufundishwa na kusaidiwa kusajili biashara zao.
Prof. Mori amehitimisha kwa kuwashauri watumishi wa BRELA kutokuishia kutoa huduma bora kwenye maonesho tu, bali kuendelea kutoa huduma bora, nzuri na kwa haraka wakati wote. Pia watambue kuwa kila mteja anayefika kupata huduma ni wa thamani, hivyo kazi ifanyike kwa ufanisi na haraka na kila anayetoka katika uwanja aondoke kwa furaha.
Akiwa katika mabanda ya BRELA pia alikabidhi vyeti vya usajili papo kwa papo kwa baadhi ya wadau waliokamilisha taratibu za usajili.