Habari
MBUNGE KANYASU ARIDHISHWA NA UTENDAJI WA BRELA MAONESHO YA MADINI GEITA
MBUNGE KANYASU ARIDHISHWA NA UTENDAJI WA BRELA MAONESHO YA MADINI GEITA.
Mbunge wa Jimbo la Geita Mjini, Mhe. Constantine Kanyasu ameridhishwa na utendaji kazi wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), kutokana na jitihada inazozifanya za kuwezesha wananchi kurasimisha biashara zao na namna inavyotoa huduma katika Maonesho ya sita (6) ya Kimataifa ya Teknolojia ya Madini 2023, yanayoendelea Mjini Geita.
Akiwa katika banda la BRELA tarehe 26 Septemba, 2023, Mhe. Kanyasu amepokelewa na Mkuu wa Sehemu ya Majina ya Biashara wa BRELA, Bw. Harvey Kombe ambaye amemueleza majukumu yanayofanywa na Taasisi hiyo, ikiwa ni pamoja na Usajili wa Majina ya Biashara na Kampuni, Usajili wa Alama za Biashara na Huduma, Utoaji wa Hataza, utoaji wa Leseni za biashara kundi “A”, Leseni za Viwanda sambamba na Usajili wa Viwanda vidogo.
Akitoa maelezo hayo kwa Mhe. Kanyasu, Bw. Kombe ameeleza kuwa katika maonesho hayo, mbali na kutoa elimu pia wamekuwa wakitoa usaidizi kwa wadau mbalimbali kwenye Mfumo wa Usajili kwa njia ya Mtandao, pamoja na kutoa huduma za usajii za papo kwa papo.
“Huduma zote za BRELA zinatolewa kwa njia ya mtandao, hivyo baadhi ya wananchi wamekuwa wakipata changamoto katika kupata huduma hizo, uwepo wetu hapa ni kuwawezesha kupata huduma hizo papo kwa papo”, amesema Bw. Kombe.
Katika maonesho hayo pia maafisa wa BRELA wamepata fursa ya kutembelea mabanda ya washiriki wengine na kuwahamasisha kurasimisha biashara zao.
Maonesho hayo ya siku 10 yalianza rasmi tarehe 20, Septemba, 2023 na yanatarajia kuhitimishwa tarehe 30 Septemba na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan.