Habari
MADIWANI WATAKIWA KUHAMASISHA URASIMISHAJI BIASHARA
MADIWANI WATAKIWA KUHAMASISHA URASIMISHAJI BIASHARA
Madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi, wametakiwa kuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha urasimishaji wa biashara kwa wananchi katika maeneo yao.
Wito huo umetolewa tarehe 24 Februari, 2023 katika Halmashari hiyo na Afisa Leseni kutoka Wakala wa Usajili na Biashara (BRELA), Bw. Koyani Aboubakari kwenye Mkutano wa Baraza la Madiwani uliofanyika katika ukumbi wa Mkutano uliopo Bariadi Sekondari.
Awali Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi, Bw. Elias Masanja aliipongeza BRELA kwa jitihada ilizofanya za kuwafikia wajasiriamali na wafanyabiashara katika maeneo yao na kuwapa elimu ya urasimishaji, itakayowawezesha kukuza biashara zao.
“Ni hatua kubwa sana ambayo BRELA mmechukua, katika mkoa huu wapo wafanyabiashara wengi ambao wanatamani kurasimisha biashara zao na kwa ujio wenu watanufaika kwa kuzirasimisha biashara zao, kupata fursa mbalimbali kutoka serikalini na sekta binafsi zinazoambatana na urasimishaji wa biashara”, amesema Bw. Masanja.
Akiwasilisha mada katika mkutano huo, Bw. Aboubakari ameeleza kuwa huduma zinazotolewa na BRELA zinamhusu kila mwananchi, hazitolewi kwa wafanyabiashara wakubwa pekee bali hata wajasiriamali wadogo na wafanyabiashara wa aina zote.
“Urasimishaji wa biashara haulengi wafanyabiashara wakubwa pekee, huduma inatolewa kwa wajasiriamali na wafanyabiashara wa ngazi zote.
Mathalani usajili wa Jina la Biashara ni shilingi Elfu Ishirini tu (20,000), usajili wa Kampuni kwa kiwango cha chini ada ya usajili ni Laki moja na Elfu Sitini na Saba na Mia Mbili (167,200) na usajili wa Kiwanda chenye kiasi cha uwekezaji usiozidi Milioni Tano (5,000,000) ni Elfu Kumi (10,000)”, ameeleza Bw. Aboubakari.
Ametoa wito kwa Madiwani wa Halmashari wa Mji wa Bariadi kuwafikishia ujumbe huo wananchi na kuwahamasisha kurasimisha biashara zao kwa mujibu wa sheria.
BRELA inatekeleza zoezi la uhamasishaji na utoaji wa elimu kwa umma kwa siku tatu katika wilaya hiyo kuanzia tarehe 23 hadi 25 Februari, 2023 na na kisha kuhitimishwa Kahama, Shinyanga 27 Februari hadi tarehe 1 Machi, 2023.