Habari
MAAFISA WA BRELA WATAKIWA KUJILINDA DHIDI YA MAGONJWA MBALIMBALI
MAAFISA WA BRELA WATAKIWA KUJILINDA DHIDI YA MAGONJWA MBALIMBALI
Maafisa wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) wametakiwa kuzingatia kanuni za afya Ili kujiepusha na magonjwa yanayoambukiza na yasiyoambukiza.
Wito huo umetolewa na wataalumu wa afya wakati wa mafunzo yaliyotolewa kwa watumishi wa BRELA kuhusu UKIMWI na magonjwa sugu yasiyoambukizwa mahala pa kazi pamoja na elimu juu ya Afya ya Akili yaliyofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Taifa Cha Utalii, Dar es Salaam, Novemba 18, 2023.
Akizungumza kuhusu Afya ya Akili, Daktari Bingwa Mwandamizi wa Afya ya Akili kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Dkt. Frank Masao amesema kwakuwa afya ni hali ya ukamilifu kimwili, kiakili na kijamii hivyo afya njema ni pamoja na kuwa na afya ya akili.
Dkt. Masao amesema changamoto ya Afya ya Akili inaweza kudhibitiwa,hivyo watumishi wanatakiwa kuangalia mienendo ya maisha yao ya kila siku Ili kuepuka msongo unaotokana na matokeo, shinikizo, mazingira magumu na hisia za mvutano.
Amefafanua kuwa changamoto ya Afya ya Akili inatokea mtu anapokabiliwa na msongo kuliko uwezo wake, hivyo inapotokea hali hiyo mwenye changamoto asisite kufika hospitali kwa ajili ya kupata tiba na ushauri wa kitabibu Ili kurejea katika hali ya kawaida.
Pia amesisitiza juu ya kuepuka matumizi ya vilevi kupindukia na tabia zingine hatarishi ambazo husababisha baadhi ya watu kupata changamoto ya Afya ya Akili na kushindwa kutekeleza majukumu yao ya kazi.
Kwa upande wa Daktari Bingwa wa magonjwa yasiyoambukizwa Dkt. Richard Murihano ameeleza namna ambavyo watumishi wanaweza kuepuka kupata magonjwa hayo kwa kuzingatia lishe bora na mpangalio sahihi wa chakula.
Aidha, wamekumbushwa kuhusu umuhimu wa kufanya mazoezi, angalau mara tatu kwa wiki ili kujiepusha na magonjwa yasiyoambukiza.
Awali, akifungua mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Huduma na Uwezeshaji wa BRELA Bw. Daimon Kisyombe amesema kuwa Taasisi imeandaa mafunzo hayo, Ili watumishi wawe na afya njema wakati wote.
“Taasisi ina watumishi wengi vijana ambao wana tabia nyingi hatarishi ikiwa ni pamoja na ulaji usiozingatia kanuni za afya hivyo, ni muhimu kuwajengea ufahamu kuhusu masuala ya afya,” amefafanua Bw. Kisyombe.
Aidha, Bw. Kisyombe amesema azma na dhamira ya Serikali ni kupambana na UKIMWI na magonjwa sugu yasiyoambukizwa, hivyo katika Mpango Mkakati ya Taasisi wa mwaka 2021/2022 hadi 2025/2026 suala hili limepewa kipaumbele lengo likiwa ni kumlinda mtumishi, familia na kuepuka hasara kwa Taifa.
Watumishi hao mbali ya kupata elimu, pia wamepata fursa ya kupima afya zao ikiwa ni pamoja na VVU, Kisukari, Shinikizo la Damu pamoja na uzito.
BRELA imejiwekea utaratibu wa kuendesha mafunzo ya mara kwa mara kwa watumishi wake juu ya masuala mbalimbali ikiwemo afya kwa lengo la kuwajengea uwezo na uelewa kwa ajili ya ustawi wa watumishi.