Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni

Tunaipa Uhai wa Kisheria Biashara yako

Habari

DC AHIMIZA WAJASIRIAMALI KURASIMISHA BIASHARA


 

DC AHIMIZA WAJASIRIAMALI KURASIMISHA BIASHARA

Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Mhe. Hashim Komba amewataka wajasiriamali wanaoshiriki katika maonesho ya Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni, (BRELA) na wadau wake kutumia fursa hiyo kurasimisha biashara zao ili biashara zao ziweze kukua.

Mhe. Komba ametoa rai hiyo  Oktoba 24, 2023 wakati akifungua Maonesho ya kwanza ya BRELA na wadau wake, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, kwenye viwanja vya Mlimani City jijini Dar es Salaam.

“Wito wangu kwenu BRELA na wadau wengine wa maonesho haya ni kwamba tuhakikishe hawa wajasiriamali mbalimbali wanakua, hivyo wasaidiwe kwa kupatiwa elimu ili waweze kurasimisha biashara zao,” amesema Mhe. Komba.

Amesema ili kuboresha zaidi maonesho haya BRELA iendelee kuandaa maonesho kama haya katika maeneo mengine yatakayowezesha wadau wengi zaidi kufikiwa. Ameyataja maeneo ambayo yana idadi kubwa ya wajasiriamali katika Wilaya ya Ubungo kuwa ni Mbezi na Manzese, hivyo BRELA itoe kipaumbele kwa kuwapatia elimu kupitia maonesho kama haya.

Pia ameitaka BRELA kuimarisha mahusiano na mazuri na taasisi zingine za Serikali hususan Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) na Serikali za Mitaa ambazo ndizo zinazowakutanisha wafanyabiashara wadogo, wa kati na wakubwa.

Mhe. Komba amesema Maonesho haya pia yatumike kufanya tathmini ya huduma zinazotolewa sambamba na kuwa na madawati yanayowakutanisha wadau ili kupunguza watu wa kati (Vishoka) ambao wamekuwa kikwazo kikubwa kwa wafanyabiashara.

“BRELA, Tume ya Ushindani (FCC), Shirika la Viwango Tanzania(TBS) pamoja na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) shirikianeni katika utoaji wa elimu ili kudhibiti na kupambana na Bidhaa bandia, kuthibitisha ubora wa bidhaa zinazozalishwa na wajasiriamali na kuhakikisha wanafanya sajili mbalimbali na kupata leseni," amesema Mhe. Komba.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA Bw. Godfrey Nyaisa amesema BRELA itaendelea kuwahamasisha wadau wake kurasimisha biashara zao kupitia majukwaa mbalimbali ikiwa ni pamoja na kushiriki katika maonesho.
Maonesho ya BRELA na wadau wake ambayo yatahitimishwa na mkutano wa Wadau tarehe 27 Oktoba, 2023, kauli mbiu yake ni "Urasimishaji Bashara katika Mapinduzi ya Nne ya Viwanda."