Habari
TIC YAKUTANA NA WAKUU WA TAASISI ZA HUDUMA ZA MAHALA PAMOJA KUJADILI NAMNA YA KUBORESHA HUDUMA KWA WAWEKEZAJI
Na Mwandishi wetu:
Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimekutana na wakuu wa Taasisi zinazounda huduma ya mahala pamoja ili kuendelea kujadili mikakati ya uboreshaji wa huduma kwa wawekezaji. Kikao hicho kimefanyika katika ukumbi wa Mahakama Kuu mjini Morogoro.
Godfrey Nyaisa Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA amesema majadiliano yalikuwa juu ya namna bora ya kufanya maboresho ya Mfumo wa huduma kwa wawekezaji kupitia dirisha la mahala pamoja “One Stop Facilitation Center”. Mkutano huu unawakutanisha Wakuu wa Taasisi kwa ajili ya kuboresha mfumo huo wa uwekezaji mkoani Morogoro, ikiwa ni mwendelezo wa vikao vya kuimarisha sekta ya uwekezaji nchini.
“Kukamilika kwa maboresho ya Mfumo wa Uwekezaji unaohusisha Taasisi mbalimbali zinazosimamia Sekta ya Uwekezaji hapa Nchini, kutachagiza ukuaji wa sekta hiyo”. amesema Nyaisa.Ameongeza kwa kusema kuwa, matarajio ya kutumia mfumo huo ni kuongeza idadi ya wawekezaji na kukuza uchumi pamoja na kupunguza mizunguko ya mchakato wa ukusanyaji wa taarifa za mwekezaji, ili kukabiliana na hali ya wawekezaji kuomba nafasi ya kuwekeza kwenye mataifa mengine ya jirani.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma kwa Wawekezaji Ndg. John Mnali amesema kukutana kwa Taasisi zinazohusika na utoaji vibali mbalimbali kwa wawekezaji ikiwemo sekta ya ardhi kutarahisha kupunguza malalamiko ya ucheleweshaji wa vibali hivyo, ambapo kwasasa zoezi zima litafanyika kwa njia ya mtandao, lengo ni mchakato wa uratibu wa taarifa kukamilika kwa siku moja.
“Mwanzoni ilikuwa ikiwachukuwa wawekezaji mpaka siku saba au hata na zaidi kupata vibali hivyo lakini sasa kuna mabadiliko makubwa na lengo letu ni Mwekezaji aweze kupata vibali vyote kwa siku moja kama atakuwa amekamilisha nyaraka zote zinazohitajika”, amesema Mnali.
Kikao hicho cha majadiliano ya kuboresha mfumo wa uwekezaji kimehusisha Wakuu wa Taasisi mbalimbali ikiwemo Mamalaka ya Mapato Tanzania (TRA), BRELA, Uhamiaji, Wizara ya Ardhi, Mamlaka ya Dawa na vifaa tiba (TMDA), Baraza la Taifa la uhifadhi wa mazingira (NEMC), Shirika la viwango Tanzania (TBS), Shirika la umeme Tanzania (TANESCO) pamoja na Baraza la Taifa la biashara (TNBC).
Pichani ni baadhi ya Wakuu wa Taasisi na Wawakilishi wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kuhudhuria mkutano wa kuboresha huduma za pamoja zinazoratibiwa na TIC kwaajili ya wawekezaji.