Habari
BRELA YATOA WITO KWA WABUNIFU
BRELA YATOA WITO KWA WABUNIFU
Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), imeshiriki maadhimisho ya Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu yanayofanyika katika uwanja wa shule ya Popatlal mkoa wa Tanga.
Katika maadhimisho hayo wadau mbalimbali wa ubunifu wameelekezwa kuhusu huduma zinazotolewa na BRELA, haswa juu ya Alama za Biashara na Huduma pamoja na Hataza.
Awali akielezea huduma zinazotolewa na BRELA kwa wabunifu walio tembelea banda la BRELA katika viwanja vya Shule ya Popatlal, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Hataza Bi. Neema Kitala amewataka wabunifu hao wasisite kusajili na kulinda bunifu zao kisheria ili zisiibiwe wala kutumika visivyo halali.
Aidha Afisa Sheria kutoka BRELA Bw. Calvin Rwambogo amewahimiza wabunifu hao kuchukua hatua ya kuanza mchakato wa kusajili Bunifu zao BRELA kabla ya kupeleka bunifu hizo katika jamii au kuingiza bidhaa zinazotakana na ubunifu wao sokoni ili kuepuka kuibiwa Bunifu hizo lakini pia hasara zinazoweza kujitokeza ikiwa ubunifu hautakuwa umesajiliwa na kulindwa kisheria.
Naye Msaidizi wa Usajili Mwandamizi Bw. Nasoro Mtavu ametoa wito kwa wabunifu kujitokeza kwa wingi ili kuhakikisha wanapata elimu ya namna bora ya kusajili na kulinda bunifu zao kisheria.
Maadhimisho ya Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu Jijini Tanga yamefunguliwa rasmi leo tarehe 27 Mei, 2024 ambapo BRELA imejipanga kutoa elimu ya Miliki Ubunifu pamoja na kusajili bunifu mbalimbali.