Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni

Tunaipa Uhai wa Kisheria Biashara yako

Habari

BRELA YATOA ELIMU KWA WADAU WA UWEKEZAJI, WANAFUNZI WA VYUO VIKUU


BRELA YATOA ELIMU KWA WADAU WA UWEKEZAJI, WANAFUNZI WA VYUO VIKUU

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), imetoa elimu kwa wadau wa uwekezaji na baadhi ya Wanafunzi wa vyuo vikuu nchini juu ya Usajili wa Makampuni na Majina ya Biashara lengo likiwa ni kuwahamasisha juu ya umuhimu wa kurasimisha biashara.


Katika semina hiyo iliyofanyika leo tarehe 12 Mei, 2023 katika ukumbi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), jijini Dar es Salaam, Afisa Usajili kutoka BRELA, Bw. Greyson Moshi amewaelimisha wadau hao juu ya umuhimu wa urasimishaji wa biashara na kuwaeleza taratibu za kusajili kampuni na majina ya.Biashara.

Bw. Greyson amezitaja aina tatu za kampuni zinazosajiliwa BRELA kuwa ni Kampuni za nje (Foreign Company), Kampuni binafsi (Private Company), na Kampuni za Umma (Public Company), sambamba na kueleza taratibu za usajili wa kampuni ambao unafanyika kwa njia ya mtandao wa (ORS) unaopatikana katika tovuti ya BRELA kupitia www.brela.go.tz

Semina hiyo imehudhuriwa na wadau wa uwekezaji, watu binafsi wenye kampuni na wanafunzi kutoka Chuo kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine(SUA).

Mwenyekiti wa Umoja wa Uwekezaji na Wajasiriamali nchini Bw. Sebastian Kingu amewasisitiza vijana kutumia fursa ya kujiunga katika umoja ili kufungua kampuni zao binafsi zitakazowawezesha kujikwamua kiuchumi na kuendana na kasi ya mabadiliko ya Sayansi na tekinolojia.

Semina hiyo iliyondaliwa na Umoja wa Uwekezaji na Wajasiriamali nchini Tanzania ilihusu fursa za Vijana kujiunga na kufungua makampuni binafsi ili kujikwamua na changamoto za ajira nchini, sambamba na kuendana na kasi ya mabadiliko ya Sayansi na Tekinolojia.