Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni

Tunaipa Uhai wa Kisheria Biashara yako

Habari

BRELA YATAKIWA KUONGEZA KASI UTOAJI WA ELIMU


BRELA YATAKIWA KUONGEZA KASI UTOAJI WA ELIMU

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) imetakiwa kuongeza kasi ya utoaji wa elimu kwa wafanyabiashara kuhusu huduma inazozitoa ikiwa ni pamoja na matumizi ya Mfumo wa Usajili kwa njia ya Mtandao (ORS), ili kutatua changamoto zinazojitokeza kwa baadhi ya wafanyabiashara kushindwa kutumia mfumo huo.

Wito huo umetolewa leo Januari 25, 2024 na Jaji Mfawidhi Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina alipotembelea banda la BRELA katika maonesho yanayoambatana na Maadhimisho ya Wiki ya Sheria katika viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam.

Amesema kuwa BRELA ni kiungo muhimu katika uanzishaji wa biashara nchini, hivyo licha ya kazi kubwa inayofanya haina budi kuongeza kasi ya utoaji elimu Ili wadau wanufaike na uwepo wa Taasisi.

Mhe.Dkt. Mlyambina ameongeza kuwa kumekuwa na uelewa mdogo wa utumiaji wa mfumo wa BRELA na kusababisha baadhi ya maombi kutokamilika kwa wakati, hivyo ni muhimu kuongeza nguvu katika utoaji elimu.

“Mmekuwa watendaji wazuri sana kwenye upande wa utoaji wa huduma kwa njia ya mtandao , hivyo maadhimisho haya yakawe chachu kwa wafanyabiashara na wadau kwa ujumla ya kurasimisha biashara zao na kutatua changamoto za kisheria,” amesema Mhe.Dkt. Mlyambina

Pia ameongeza kwa kuwataka wadau mbalimbali kutembelea maonesho hayo na kufika katika banda la BRELA kurasimisha biashara zao pamoja na kutatua changamoto mbalimbali kwani huduma zinatolewa papo kwa papo.

Maonesho hayo yaliyoanza Januari 24, 2024 yatahitimishwa Januari 30, 2024.