Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni

Tunaipa Uhai wa Kisheria Biashara yako

Habari

BRELA YAPONGEZWA KWA UTENDAJI MZURI


 

BRELA YAPONGEZWA KWA UTENDAJI MZURI

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo imetoa pongenzi kwa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) kutokana na mabadiliko mbalimbali ya utendaji kazi yanayofanyika katika Taasisi hiyo.

Hayo yamebainishwa tarehe 09 Novemba, 2023 na Mwenyekiti Kamati hiyo Mhe. Deo Mwanyika (Mb)wakati wa Semina Maalumu iliyoandaliwa na BRELA jijini Dodoma kuwaelimisha wajumbe wa Kamati hiyo majukumu yanayofanywa na Taasisi hiyo.

Bw. Mwanyika amesema changamoto zilizokuwepo awali za kiutendaji kwa sasa hazipo na matokeo yake BRELA inaendelea kufanya kazi kwa weledi na uadilifu.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe (Mb), akimwakilisha Waziri wa Wizara hiyo amesema, elimu zaidi inapaswa kutolewa ili kuwa na uelewa mpana kuhusu majukumu yanayofanywa na BRELA.

“Kama mnavyoona kuna baadhi ya mambo mliyoyaeleza hapa Waheshimiwa Wabunge ndiyo wanayasikia hivyo semina hizi ni muhimu kufanyika mara kwa mara pamoja na kuwa na muda wa kutosha,” ameeleza Mhe. Kigahe.

Awali Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA aliwaeleza wajumbe Kamati hiyo kuwa BRELA inaendelea kufanya maboresho mbalimbali ya kimifumo lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa wadau wanapata huduma za BRELA kwa urahisi zaidi.

Amewahakikishia kuwa taarifa za wadau wote waliofanya sajili mbalimbali BRELA ambazo zinafanyika kwa njia ya mtandao zipo salama na Taasisi imekuwa ikishirikiana na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) kuhakikisha kuwa mfumo unakuwa salama wakati wote.

Kwa upande wake Mjumbe wa Kamati Mhe. Prof. Sospeter Muhongo(Mb) alitaka kufahamu kama BRELA ina mpango wowote wa kuwasaidia wabunifu waliojisajili BRELA kwa kuwatafutia masoko ya Bunifu zao.

Akitoa ufafanuzi Msajili Msaidizi Mkuu wa BRELA Bw. Seka Kasera amesema Wizara ya Viwanda na Biashara ilianza mchakato wa kuwa na Sera ya Taifa ya Miliki Ubunifu ambapo maoni ya wadau yameshachukuliwa na sasa Sera hiyo iko hatua ya mwisho na itakapokamilika itawezesha kuwapatia masoko wabunifu mbalimbali ambao wamesajili bunifu zao BRELA.

Bw, Seka amesema kuwa Sheria iliyopo sasa inaiwezesha BRELA kutoa linzi pekee kwa Bunifu mbalimbali.

“Sheria ya Miliki Ubunifu itakapofanyiwa marekebisho haitaishia kuweka linzi pekee bali itahakikisha kuwa bunifu hizo zinaingia sokoni ili wabunifu waweze kunufaika na bunifu zao”, amefafanua Bw, Seka.

Naye Mjumbe wa Kamati hiyo Mhe. Abdul-Aziz Abood alitaka kufahamu BRELA inashugulikiaje suala la ufanano wa majina ya Kampuni na ya Biashara wadau wanapopeleka maombi ya majina yanayofanana.

Akifafanua kuhusu hoja hiyo Msajili Msaidizi wa BRELA Bi. Leticia Zavu amesema vigezo vinavyotumika katika usajili wa Kampuni na Majina ya Biashara ni kutokuwa na ufanano wa matamshi na maandishi hivyo aliyesajiliwa awali ndiye hulindwa na kuendelea kutumia jina husika.

Katika semina hiyo BRELA iliwasilisha mada kuhusu utekelezaji wa Sheria ya Usajili ya Kampuni na Majina ya Biashara, Sheria ya Leseni za Biashara na Viwanda pamoja na Sheria ya Usajili wa Alama za Biashara na Huduma.