Habari
BRELA YAKUTANA NA WADAU WA SEKTA BINAFSI
BRELA YAKUTANA NA WADAU WA SEKTA BINAFSI
Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), imekutana na wadau wa sekta binafsi na kuwajengea uwezo kuhusu dhana ya Kanuni za Wamiliki Manufaa wa Kampuni zinazomilikiwa na Wabia kwa lengo la kuelekezana mabadiliko ya sheria na kupokea uzoefu kutoka kwa wabobezi wa masuala ya sheria na biashara.
Akifungua warsha ya siku moja katika ukumbi wa Ngorongoro Jijini Arusha, leo tarehe 9 Machi, 2023 kwa niaba ya Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA Bw. Godfrey Nyaisa, Kaimu Mkuu wa Sehemu ya Makampuni, Bw. Isidory Nkindi, ameeleza kuwa Kanuni za Wamiliki Manufaa zinataka Kampuni kuwasilisha taarifa za Wamiliki Manufaa wa mwisho katika Kampuni.
Ameeleza kuwa Wamiliki Manufaa ni wale wenye manufaa kwenye kampuni kwa kumiliki hisa, haki ya kupiga kura na kutoa maamuzi kwenye uendeshaji wa kampuni.
“Kama mnavyojua, Bunge la Jamhuri Muungano wa Tanzania kupitia Mswada wa Sheria ya Fedha, ya mwaka 2020, lilipitisha marekebisho ya Sheria ya Makampuni, Sura ya 212 kwa lengo la kuwezesha upatikanaji wa taarifa za Wamiliki Manufaa (beneficial owners) katika kampuni ambazo ni muhimu katika kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara, sababu za kikodi pamoja na kudhibiti utakatishaji wa fedha haramu na ufadhili wa vitendo vya ugaidi”, amefafanua Bw. Nkindi.
Pia amesema kupitia majadiliano haya, BRELA inatarajia kuwa na mjadala mpana wenye lengo la kuboresha hasa kwenye maeneo ya “Substantial Control” na kampuni za kigeni ambayo tayari yameshaanza kuleta tafsiri kinzani.
"Ni matarajio ya Taasisi kuwa elimu hii itawawezesha kuwa mabalozi wazuri katika utekelezaji wa sheria kwakuwa mnawahudumia wenye Kampuni, hivyo ni vema mkatoa ushauri kwa usahihi", amesisitiza Bw. Nkindi.
Kwa upande wake, wakili wa kujitegemea kutoka Chama cha Mawakili, Bi. Fauzia Mustapha amehitimisha kwa kusema kuwa warsha hiyo imekuwa ya manufaa kwakuwa kanuni hizo ni mpya hivyo watafahamu kwa undani kuhusu dhana nzima na namna ya kuwasilisha taarifa kwenye mfumo pamoja na kushauri maboresha kwenye kanuni zilizopitishwa ili kuwa rafiki katika kuhudumia umma.
Wadau walioshiriki warsha hii ni wafanyabiashara, Taasisi za Fedha, Wanasheria, Wahasibu, waliosajiliwa kusaidia kampuni kwenye masuala ya ushauri, kisheria na kimahesabu na kuwasilisha taarifa zao.