Habari
BRELA YAIKABIDHI CHANETA VIFAA YA MICHEZO
BRELA YAIKABIDHI CHANETA VIFAA YA MICHEZO
Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), imekabidhi vifaa vya michezo truck suits jozi 25 pamoja na mipira mitano kwa Chama cha Netiboli Tanzania (CHANETA) vitakavyotumiwa na timu ya netiboli Wanawake, Taifa Queens.
Akikabidhi vifaa hivyo leo tarehe 22 Novemba, 2023, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA Bi. Loy Mhando amesema BRELA ni mdau mkubwa wa michezo, kwakuwa inatambua kuwa michezo ni afya, ni burudani pia kupitia michezo Taasisi inajitangaza na zaidi ya hapo michezo ni biashara hivyo kama Taasisi inayohusika na masuala ya urasimishaji biashara ina wajibu wa kushirikiana na wana michezo nchini.
"BRELA imekuwa ikishiriki katika michezo mbalimbali na kutoa misaada kwa wadau wa michezo ili kuhakikisha kuwa sekta ya michezo nchini inakuwa na kujipambanua kimataifa", amefafanua Bi. Mhando.
Aidha Bi. Mhando amesema msaada wa vifaa uliotolewa unaunga mkono jitihada za Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuhamasisha ukuaji wa sekta ya michezo nchini.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa CHANETA, Bi. Rose Mkisi ameishukuru BRELA kwa msaada wa vifaa vya michezo kwa timu ya Taifa Queens .
“Tunaishukuru sana BRELA kwa msaada wa vifaa vya michezo na tunaahidi kupitia vifaa hivi vya michezo timu ya Netiboli itafuzu vyema katika michuano mbalimbali watakayoshiriki.
BRELA imetoa msaada wa vifaa hivyo baada ya kupokea maombi kutoka CHANETA kuhusu uhitaji wa vifaa vya michezo vitakavyotumika katika mashindano mpira wa pete nchini Botswana.
Hafla hiyo ya makabidhiano ya vifaa vya michezo imefanyika katika Ofisi za BRELA jijini Dar es Salaam.