Habari
BRELA YAIBUKA KIDEDEA DHIDI YA HAZINA
BRELA YAIBUKA KIDEDEA DHIDI YA HAZINA
Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), inayoshiriki katika mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali Tanzania (SHIMIWI) imeibuka kidedea baada ya timu ya mpira wa miguu (wanaume) kuinyuka timu ya Hazina bao moja kwa nunge.
Pambano hilo limefanyika leo tarehe 29 Septemba, 2023 katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE), mkoani Iringa.
Kwa upande wa wanawake timu ya mpira wa pete ya BRELA
imechuana vikali na timu ya wanawake kutoka ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Lindi na kujiibulia magoli 10 huku wapinzani wao wakiongoza kwa goli 19, katika pambano lililofanyika katika viwanja vya Ruaha mjini humo.
Mashindano hayo yaliyoanza leo yameamsha ari kwa timu za BRELA ambazo zimepania kuondoka na ushindi wa kishindo.
Michezo inayoandaliwa na SHIMIWI inalenga kuimarisha Afya za watumishi na kuongeza ufanisi mahala pa kazi na kuwajengea mahusiano mazuri baina yao.
Kauli mbiu ya mwaka huu inasema "Michezo mahala pa kazi huimarisha afya na kuongeza ufanisi kazini”, hivyo watumishi wanapaswa kulinda afya zao kwa kufanya mazoezi, vilevile kutengeneza mahusiano baina ya watumishi kutoka Wizara na Taasisi mbalimbali.
Mashindano haya ya siku 14 yatashirikisha watumishi wa Serikali kutoka Wizara, Idara za Serikali pamoja na Taasisi.
Mashindano hayo ya siku 14 yanatarajiwa kufunguliwa rasmi tarehe 4 Oktoba, 2023 katika uwanja wa Samora mjini humo siku ya tarehe 4 Oktoba, 2023.
Wanamichezo zaidi ya 2000 kutoka timu zaidi ya 70 zinazoundwa na watumishi wa serikali kutoka wizara mbalimbali, idara zinazojitegemea na wakala wa serikali wanashiriki.