Habari
BRELA YAELEKEZWA KUWALEA WAFANYABIASHARA
BRELA YAELEKEZWA KUWALEA WAFANYABIASHARA
Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), imeelekezwa kuwalea wafanyabiashara nchini kwa kurahisisha jinsi ya kuifikia, kuwa mbunifu wa namna ya kuwahudumia na kuifanya Taasisi kuwa ya watanzania ili kufikia malengo ya uanzishwaji wake.
Maelekezo hayo yametolewa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji alipokuwa akifungua mkutano wa kwanza wa BRELA na wadau wake leo tarehe 27 Oktoba, 2023 kwenye ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.
Mhe. Dkt. Kijaji ameeleza kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameamua kukabidhi uchumi wa taifa kwa sekta binafsi na amefungua mipaka yote, hivyo taasisi ya kwanza inayoshughulikia sekta binafsi ni BRELA kwakuwa uchumi wa nchi unakua kupitia ukuaji wa sekta ya viwanda na biashara nchini.
Ameongeza kwa kusema kuwa kuanzia mwaka 2019 hadi Juni, 2023 Serikali imeeendelea kutekeleza mpango wa kuboresha mazingira bora ya biashara na kuondoa tozo na kodi mbalimbali zaidi ya 374 zilizosumbua wafanyabiashara ambapo Serikali imefikia zaidi ya asilimia 75 ya dhamira yake.
“Kwa mwaka wa fedha 2023/2024 kupitia Sheria ya Fedha jumla ya Sheria na Kanuni 13 na pia Sheria ya Fedha ya mwaka 2023 zimeweza kupunguza na kufuta tozo, ada na faini 67 ikiwa na lengo la Serikali ya awamu ya sita la kuhakikisha mazingira ya biashara kuwa bora zaidi”, ameeleza Mhe. Dkt. Kijaji.
Mhe. Dkt Kijaji amesisitiza kuwa hakuna uchumi wa nchi unaokua kama hakuna maendeleo katika sekta ya viwanda na ya biashara iliyo imara, Serikali inahakikisha inaboresha mazingira ya ufanyaji biashara ndani na nje ya Tanzania na taasisi za udhibiti hazitumii mamlaka zao kufungia biashara yoyote lengo ni kuhakikisha kuwa sekta ya biashara inalea uchumi wa nchi.
Ameendelea kusema kuwa anatambua kuwa wafanyabiashara wapo mbele zaidi, kwa kuwa dunia haiwezi kutusubiri hivyo kwa kasi hiyo Wizara ya Viwanda na Biashara imeweka dhamira ya kuboresha Sera na Sheria ili zisomane na mabadiliko ya uchumi.
“Tunaangalia uwekezano wa kutoa leseni zote za biashara katika mfumo mmoja wa BRELA kuliko kuwa na mifumo mingi inayotoa huduma za leseni za biashara hii itasaidia uratibu mzuri wa leseni za biashara na Serikali kuwa na kanzi data moja ya taarifa za biashara, tunawaomba mtupe ushirikiano katika hatua hii ili kuwahudumia kwa ufanisi mzuri", ameongeza Mhe.Dkt Kijaji.
Mhe. Dkt. Kijaji amehitimisha kwa kuielekeza BRELA kutumia mkutano huu kama sehemu ya kupokea maoni ya Watanzania, kuboresha na kutumia vema maoni hayo na kila mwaka mkutano mtakapokutana na wadau hawa muwe na mijadala yenye majibu ya utatuzi wa changamoto zao
Nae Mbunge wa Kahama Mjini, Mhe. Jumanne Kishimba akiongea kwa niaba ya wafanyabiashara walioshiriki mkutano huo amesema wafanyabiashara wengi hukimbilia huduma za BRELA ili kupata huduma za mikopo kutoka taasisi za fedha na kupata zabuni ila wengi hawaelewi tafsiri za kisheria za kampuni, hivyo ameishauri kuweza kuzitafsiri kwa lugha nyepesi ili kuepusha migogoro mbalimbali.
Awali katika hotuba yake, Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Godfrey Nyaisa ameeleza kuwa anatambua kuna sheria nyingi ambazo zimepitwa na wakati na ipo kwenye hatua za maboresho ya sheria mbalimbali kama vile Maboresho ya Sheria ya Viwanda ya mwaka 1967, Maboresho ya Sheria ya Hataza ya Mwaka 1987, Maboresho ya Sheria ya Miliki Bunifu ya Mwaka 1986 na Maboresho ya Sheria ya Kampuni ya Mwaka 2002 ili ziendane na mabadiliko ya Kiteknolojia na ukuaji wa sekta ya biashara.
Akihitimisha Mkutano huo wa Wadau, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya BRELA, Prof. Neema Mori, amehitimisha kwa kuwaahidi wadau kuwa wamepokea maoni yote ya wadau na kuwahakikishia kuwa Bodi itasimamia Taasisi ili kuleta urahisi wa matumizi ya mifumo kuwa kidigitali na kidigiti na itaendelea kusimamia michakato ya kuwepo kwa Sera na maboresho ya sheria mbalimbali.