Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni

Tunaipa Uhai wa Kisheria Biashara yako

Habari

BRELA KUWAJENGEA UWEZO WAANDISHI WA HABARI


 

BRELA KUWAJENGEA UWEZO WAANDISHI WA HABARI

Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdallah amewashauri waandishi wa Habari za Biashara na Uchumi kuendelea kuwafikishia wananchi taarifa sahihi zinazohusu Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni-BRELA.

Ushauri huo ameutoa Juni 18, 2024 mjini Morogoro wakati wa kufungua mafunzo ya siku nne (4) ya BRELA kwa waandishi wa Habari.

Serikali kwa kupitia (BRELA) imeandaa mafunzo maalumu kwa waandishi wa habari za biashara 44 kutoka vyombo mbalimbali vya habari kutoka Mkoa wa Dar es Salaam lengo likiwa kuwajengea uwezo utakaowezesha waandishi hao kuandika kwa weledi habari za Serikali.

Amefafanua kuwa wameanza na waandishi hao wa habari za biashara kutoka Mkoa wa Dar es Salaam na hasa wanaondika habari za BRELA lakini mikakati yao ni kwamba mafunzo hayo yatatolewa kwa waandishi wa Mikoa yote na lengo ni kuhakikisha wanaendelea kuwajengea uwezo wadau muhimu wakiwemo waandishi wa habari.

Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Godfrey Nyaisa amesema sababu za mafunzo ni moja ya utekelezaji wa malengo ya Serikali ya kuhakikisha inatoa elimu kwa umma na wadau mbalimbali.

"Tumeshuhudia baadhi ya habari ambazo zinaripotiwa lakini zina makosa mengi. Namna ya kupunguza makosa hayo ya kiuandishi wa habari za Kibiashara ni kutoa elimu ya mara kwa mara kwa wanahabari ili kuondoa makosa hayo huku akisisitiza kwamba kupitia Wakurugenzi wa Wakala huo watatoa elimu ya kutosha katika mafunzo hayo na waandishi wa habari wasisite kuuliza kwa lengo la kujifunza zaidi,"amesema Nyaisa.

Aidha, amesema mpango mkakati wa BRELA ni kuwa na kanzi data ya waandishi wa habari ambao watakuwa wanaandika habari za Wakala huo ili kusaidia kuwa na habari zenye usahihi na kwamba mafunzo hayo yanaendelea kutolewa sambamba na kuwaita katika matukio yanayohusu BRELA.

Pia amesema kuanzia sasa wataanza kutoa tuzo Maalum kwa waandishi wa habari za biashara ambao watakuwa wakiandika makala zenye matokeo chanya kwa jamii lakini makala ambazo zitakuwa zimejitosheleza.