Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni

Tunaipa Uhai wa Kisheria Biashara yako

Habari

BRELA KUENDELEA KUIMARISHA UHUSIANO NA CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM (UDSM)


BRELA KUENDELEA KUIMARISHA UHUSIANO NA CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM (UDSM)

Wakala wa usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) imetoa pongezi kwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa kuadhimisha wiki ya Utafiti na Ubunifu ambayo iliambatana na Maonesho ya Tafiti na Bunifu mbalimbali zinazofanywa na wadau kutoka katika chuo hicho.

Akizungumza katika hafla ya kuhitimisha Maadhimisho hayo tarehe 07 Juni, 2024 katika Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, kwa niaba ya Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA Bi Loy Mhando ambaye ni Mkurugenzi wa Miliki Ubunifu amesema, BRELA itaendelea kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kutokana na mchango wake mkubwa wa kuendeleza Bunifu na Tafiti mbalimbali zinazofanywa na wahadhiri na wanafunzi chuoni hapo.

Katika Maadhimisho hayo yaliyohudhuriwa na viongozi, wadau wa maendeleo, wawakilishi kutoka taasisi za Umma na binafsi, wahadhiri, watumishi na wanafunzi wa kada Mbalimbali wa chuo hicho wameelezwa namna wanavyoweza kutumia bunifu zao kutatua changamoto katika jamii, vile vile kujikwamua kiuchumi na kutengeneza fursa za ajira kwa wengine.

Washiriki wamepata fursa ya Kukumbushwa kuwa nyenzo za Miliki Ubunifu ni mali kama mali nyingine na inapolindwa inakuwa na thamani inayoweza kuleta faida nyingi kwa wabunifu na Taifa kwa ujumla. Bi. Mhando ametoa rai kwa Chuo na wabunifu kuhakikisha wanalinda kazi zao kwa kupitia BRELA ili waweze kunufaika na kazi zao pamoja na kuepuka hasara ya bunifu zao kuhujumiwa na watu wengine.

Aidha, ameeleza kuwa, katika eneo la kukuza na kuhamasisha ubunifu nchini, BRELA inatekeleza jukumu muhimu kati ya majukumu yake ambalo ni ulinzi wa bunifu na kurasimisha biashara nchini kwa kusajili Kampuni, Majina ya Biashara na kutoa Leseni za Biashara, kwa kutambua hilo, BRELA imesaini hati ya makubaliano ushirikiano MoU) na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Kama sehemu ya ushirikiano huo, BRELA imeendelea kutoa ufadhili kwa wanafunzi wa Shahada ya Umahiri ya Miliki Ubunifu (Master of Intellectual Property - MIP) ambao idadi yao ni 14 mpaka toka kuanzishwa kwakwe mwaka 2020.

Katika tukio hilo muhimu la Maadhimisho ya Wiki ya Utafiti na Ubunifu, BRELA imetoa ufadhili wa Tuzo moja wapo kati ya Tuzo zilizotolewa ambayo ni katika kipengele cha ‘Mradi bora wa Ubunifu kutoka shahada ya kwanza.