Habari
BRELA ANA KWA ANA NA WAFANYABIASHARA MBEYA
BRELA ANA KWA ANA NA WAFANYABIASHARA MBEYA
Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), inafanya ukaguzi elimishi kwa kukutana na wafanyabiashara katika maeneo yao ya biashara jijini Mbeya, kwa lengo la kuhamasisha urasimishaji wa Biashara.
Katika zoezi hilo lilioanza leo Desemba 18, 2023, maafisa wa BRELA wametembelea soko la Mwanjelwa na kukutana na wafanyabiashara mbalimbali ambao wamewaelimisha kuhusu huduma za Usajili wa Kampuni na Majina ya Biashara na taratibu zingine za baada ya usajili ikiwemo uwasilishaji wa taarifa za Wamiliki Manufaa wa Kampuni.
Akizungumza na wafanyabiashara katika zoezi hilo, Afisa Usajili wa BRELA Bw. Jacob Mkuye amesema, ziara hiyo mbali na kuwaelimisha pia wanatumia fursa hiyo kutatua changamoto mbalimbali ambazo wadau wanakumbana nazo wakati wa kufanya sajili katika Mfumo wa Usajili kwa njia ya Mtandao (ORS).
Ameongeza kuwa pia watatoa usaidizi kwa wadau walioshindwa kuwasilisha taarifa za mwaka za Kampuni na kwa wale walioshindwa kuwasilisha taarifa za Wamiliki Manufaa.
Bw. Mkuye amfafanua kuwa uwasilishaji wa taarifa za Wamiliki Manufaa wa Kampuni ni zoezi endelevu liloanza tangu mwaka 2021 ambapo kampuni zinapaswa kuwasilisha taarifa za wamiliki manufaa wake kwa Msajili wa Kampuni.
Katika siku ya kwanza ya zoezi hilo BRELA imewatembelea wafanyabiashara wapatao 80. Aidha, BRELA imepanga ifikapo Disemba 22, 2023, kuwafikia wajasiriamali, wafanyabiashara na wamiliki wa kampuni kwa kuwapatia elimu ya huduma mbalimbali zinazotolewa na Taasisi.