Habari
BBT AMCOS WASHAURIWA KUSAJILI ALAMA ZA BIASHARA
BBT AMCOS WASHAURIWA KUSAJILI ALAMA ZA BIASHARA.
Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) leo Julai 07, 2024 imetoa elimu kuhusu Alama ya Biashara na Hataza kwa wanufaika zaidi ya 9 (BBT) kutoka Chinangali Dodoma ambao wametembelea banda la BRELA katika maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam Sabasaba.
Akitoka elimu hiyo, Afisa Usajili kutoka BRELA Kurugenzi ya Miliki Ubunifu Bw. Stansalaus Kigosi amewashauri wanufaika hao kuhakikisha wanasajili Alama na nembo ya biashara ili kupata ulinzi wa kisheria na kutambulisha bidhaa zao sokoni kwa urahisi.
Bw. Kigosi amesema kuwa na nembo iliyosajiliwa BRELA inamuwezesha mfanyabiashara kuitofautisha bidhaa yake na ya mtu mwingine sokoni.
Naye Mjumbe wa Bodi ya Chinangali BBT AMCOS Bi. Naomi Chabandi amesema mafunzo hayo yanakwenda kuwasaidia katika kuitambulisha biashara yao
sokoni kwakuwa wamepata uelewa wa masuala ya Usajili wa Majina ya Biashara, Alama pamoja na Huduma.
Aidha Bw. Juma Ramadhan, mwenyekiti wa habari na mawasiliano Chinangali BBT AMCOS amesema wamelazimika kutembelea BRELA ili kupata elimu kwakuwa wamedhamiria kuitangaza biashara yao katika soko la ndani na nje hivyo wanahitaji ulinzi wa kisheria kwenye kazi zao.
Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam Sabasaba msimu huu yanafanyika yakiwa na kauli mbiu isemayo "Tanzania ni Mahali Sahihi pa Biashara na Uwekezaji" na yanatarajia kuhitimishwa rasmi tarehe 13 Julai, 2024.