Habari
ACHENI KUKWEPA KUSAJILI BRELA- DC SHEKIMWERI
ACHENI KUKWEPA KUSAJILI BRELA- DC SHEKIMWERI
Wafanyabiashara wametakiwa kuacha tabia ya kufanya biashara bila kusajili Majina ya Biashara na Kampuni zao na kukwepa kulipa kodi wakidhani wananufaika bila kujua kwamba wanakosa fursa mbalimbali za maendeleo ikiwemo mikopo.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Mhe. Jabir Shekimweri tarehe 5 Desemba, 2023 jijini Dodoma, alipokuwa akifungua semina kuhusu dhana ya Wamiliki Manufaa wa Kampuni na Majina ya Biashara kwa mawakili, wahasibu, kampuni za ushauri wa biashara na wafanyabiashara.
"Kutokulipa kodi, kutokusajili kampuni kutokuwa na leseni, kufanya biashara kienyeji, unaweza ukaona ni ujanja lakini mwisho wa siku hutafanikiwa, itakunyima fursa ya kukopa, utakuwa na mapato makubwa mkononi wakati kwenye nyaraka, taarifa na kumbukumbu na rekodi za ulipaji wako wa kodi utakuwa umedanganya, kwa hiyo huwezi kupata mkopo na kubaki kuwa mlalamishi kuwa hupewi mkopo," amesema Mhe. Shekimweri.
Mhe. Shekimweri ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dodoma katika ufunguzi wa warsha hiyo amewahimiza wafanyabiashara kufanya biashara katika mazingira rasmi kwa lengo la kupata mafanikio.
Amewataka washiriki hao kutumia mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) kuzielewa Sheria na Kanuni za Umiliki Manufaa katika kampuni na utaratibu wa kuwasilisha taarifa kwa msajili wa kampuni.
Naye Mwakilishi wa Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, ambaye ni Kaimu Mkuu wa Sehemu ya Makampuni, Bw. Harvey Kombe amesema kuwa Taasisi itaendelea kukutana na wadau kwa lengo la kushauriana na kuelekezana kuhusiana na mabadiliko ya sheria mbalimbali ikiwa ni pamoja na marekebisho ya sheria ya makampuni sura namba 212 ya uwasilishaji wa taarifa za Wamiliki Manufaa.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mawakili Kanda ya Kati Dodoma, Wakili Mary Munissi ameungana na kauli ya Mkuu wa Wilaya Dodoma, Mhe.Shekimweri kwa kuwataka wateja wao kujenga tabia ya kufuata sheria na kanuni za biashara za kusajili kampuni zao na kulipa kodi kwa mujibu wa sheria.
Ametoa wito kwa mawakili kuacha tabia ya kuwakumbatia kwa kuwatetea wateja wao wanaokiuka taratibu, sheria na kanuni hizo, bali kinachotakiwa ni kuwaelimisha umuhimu wa kuzifuata bila shuruti.