Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni

Tunaipa Uhai wa Kisheria Biashara yako

Habari

MHE. DKT. BITEKO ARIDHISHWA NA HUDUMA ZA BRELA KATIKA MAONESHO YA 7 YA TEKNOLOJIA YA MADINI MKOANI GEITA


 

MHE. DKT. BITEKO ARIDHISHWA NA HUDUMA ZA BRELA KATIKA MAONESHO YA 7 YA TEKNOLOJIA YA MADINI MKOANI GEITA

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe.Dkt Doto Biteko ameipongeza na kuridhishwa na huduma zinazotolewa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), kwa kuwafikia wafanyabiashara na kutoa huduma na hamasa ya kurasimisha biashara zao.

Mhe. Dkt Biteko ameyasema hayo leo tarehe 5 Oktoba, 2024 katika uzinduzi wa Maonesho ya 7 ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini katika viwanja vya EPZA Bomba mbili mkoani Geita.

“Endeleeni na kazi nzuri mnayofanya kama taasisi” Amesema Mhe.Dkt Biteko. Maonesho haya ya madini yanaongozwa na kaulimbiu isemayo matumizi ya teknolojia sahihi na nishati safi katika sekta ya madini kwa maendeleo endelevu.

Naye Afisa Leseni Mwandamizi kutoka Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Bw.Koyan Aboubakar akitoa maelezo na lengo la kushiriki maonesho haya kwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt Doto Biteko alipotembelea banda la BRELA amebainisha kwamba Dira ya BRELA hivi sasa ni kuwafikia wadau wengi zaidi pamoja na kutoa huduma za papo kwa papo kwa wananchi wa mkoa wa Geita.

“Ushiriki wetu katika maonesho kama haya ni kuhakikisha huduma zote za BRELA za Usajili wa Majina ya Biashara, Usajili wa Kampuni, Usajili wa Alama za Biashara na Huduma, Usajili wa Hataza, Utoaji wa Leseni za Biashara kundi “A”, Usajili wa Kiwanda na huduma za kulipia ada za mwaka na uhuishaji wa taarifa za Biashara na Makampuni zinatolewa papo kwa papo.

Banda la BRELA ni miongoni mwa mabanda ya taasisi za Serikali ambazo zimeshiriki katika maonesho haya ya madini kwa lengo la kusogeza huduma kwa karibu kwa jamii hasa kwa kuzingatia kwamba huduma zote zinatolewa kwa njia ya mtandao zinapatikana papo kwa papo.

Pamoja na kutoa huduma ya papo kwa papo, pia inatoa elimu kwa umma juu ya namna ya upataji wa huduma za BRELA ambazo zinatolewa kwa njia ya mtandao.Maonesho haya ya siku kumi na moja yamefunguliwa leo tarehe 5 Oktoba, 2024 na Mhe.Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati na yatahitimishwa rasmi tarehe 13 Oktoba,2024.