Habari
MBUNGE WA BUSANDA AHIMIZA WAJASIRIAMALI KURASIMISHA BIASHARA
MBUNGE WA BUSANDA AHIMIZA WAJASIRIAMALI KURASIMISHA BIASHARA
Mbunge wa Jimbo la Busanda , Mhe. Tumaini Brygeson Magessa amewataka wajasiriamali wanaoshiriki katika maonesho ya 7 ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini katika viwanja vya EPZA Bombambili mkoa wa Geita kutumia fursa hiyo kurasimisha biashara zao ili ziweze kukua.
Mhe. Magessa ametoa rai hiyo leo Oktoba 07, 2024 wakati alipotembelea banda la Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) lililopo katika viwanja vya EPZA Bombambili mkoa wa Geita na kupata huduma ya usajili wa papo kwa papo.
Akionesha kuridhishwa na huduma zinazotolewa bandani hapo Mhe.Magessa ametoa wito kwa BRELA na wadau wengine wanaotoa huduma katika maonesho kuhakikisha wajasiriamali mbalimbali wanakua, hivyo wasaidiwe kwa kupatiwa huduma na elimu ili waweze kurasimisha biashara zao.
Pia ameipongeza BRELA kwa huduma nzuri za utoaji wa elimu pamoja na huduma ya sajili mbalimbali inazozitoa kwa kuwa zitawawezesha wafanyabiashara wadogo, wa katı na wakubwa waliojitokeza katika maonesho haya kupata huduma stahiki za urasimishaji wa biashara zao kwa urahisi.
Maonesho ya 7 ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yaliyoanza tarehe 2 Oktoba,2024 yamefunguliwa rasmi tarehe 5 Oktoba na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe.Dotto Biteko yatahitimishwa tarehe 13 Oktoba, 2024 katika viwanja vya EPZA Bombambili mkoa wa Geita, kauli mbiu ya maonesho haya ni "Matumizi ya Teknolojia na Nishati Safi katıka Sekta ya Madini kwa Maendeleo Endelevu”.