Habari
BRELA YATOA WITO KWA WABUNIFU
BRELA YATOA WITO KWA WABUNIFU
Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), imeshiriki maonesho ya 7 ya Kimataifa ya Madini yanayofanyika katika uwanja wa EPZA Bomba mbili mkoa wa Geita.
Katika maadhimisho hayo wadau mbalimbali wa ubunifu wameelekezwa kuhusu huduma zinazotolewa na BRELA, haswa juu ya Alama za Biashara na Huduma pamoja na Hataza.
Msaidizi wa Usajili kutoka BRELA Bi. Ulumbi Kulian amewatembelea baadhi ya wabunifu wanaoshiriki maonesho haya na kuwataka wabunifu hao wasisite kusajili na kulinda bunifu zao kisheria ili zisiibiwe wala kutumika isivyo halali.
Aidha Bi. Ulumbi Kulian amewahimiza wabunifu hao kuchukua hatua ya kuanza mchakato wa kusajili Bunifu zao BRELA kabla ya kupeleka bunifu hizo katika jamii au kuingiza bidhaa zinazotokana na ubunifu wao sokoni ili kuepuka kuibiwa Bunifu hizo lakini pia hasara zinazoweza kujitokeza ikiwa ubunifu hautakuwa umesajiliwa na kulindwa kisheria.
Pia ametoa wito kwa wabunifu kujitokeza kwa wingi ili kuhakikisha wanapata elimu ya namna bora ya kusajili na kulinda bunifu zao kisheria.
Maadhimisho ya 7 ya Kimataifa ya Madini mkoani Geita yanafunguliwa rasmi tarehe 05 Oktoba, 2024 ambapo BRELA imejipanga kutoa elimu ya Miliki Ubunifu pamoja na kusajili bunifu mbalimbali.