Habari
WATUMISHI WA BRELA WAPATIWA MAFUNZO YA UKIMWI NA MAGONGWA YASIOAMBUKIZWA
WATUMISHI WA BRELA WAPATIWA MAFUNZO YA UKIMWI NA MAGONGWA YASIOAMBUKIZWA
Dar es Salaam, Juni 14, 2025 – Watumishi wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) wamepatiwa mafunzo maalum kuhusu udhibiti wa Virusi vya Ukimwi (VVU), UKIMWI na magonjwa yasiyoambukizwa (NCDs), katika hatua ya kuimarisha afya na ustawi wa wafanyakazi wake.
Mafunzo hayo yametolewa na wataalamu kutoka Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS), wakiongozwa na Dkt. Hafidh Ameir pamoja na Dkt. Zainab Mwinyimkuu.
Akizungumza katika mafunzo hayo, Dkt. Hafidh Ameir alisisitiza umuhimu wa watumishi wa umma kuwa na uelewa mpana kuhusu afya zao kwa kupima mara kwa mara na kuchukua hatua stahiki za kinga dhidi ya maambukizi ya VVU na magonjwa mengine kama Homa ya Ini na Saratani ya Tezi Dume. Alisema elimu hiyo itachangia kuongeza tija mahali pa kazi kutokana na afya bora ya watumishi.
Kwa upande wake, Dkt. Zainab Mwinyimkuu aliwataka watumishi hao kuzingatia maamuzi sahihi ya kiafya, kufuata ushauri wa wataalamu na kujenga tabia endelevu ya kupima afya ili kuepuka athari za magonjwa yasiyoambukizwa.
Watumishi walioshiriki mafunzo hayo waliipongeza uongozi wa Afisa Mtendaji Mkuu Bw. Godfrey Nyaisa kwa kuweka afya ya wafanyakazi kipaumbele, wakisema elimu waliyoipata imewajengea ari ya kujitambua kiafya na kuthamini afya zao.
Mafunzo hayo ni sehemu ya mkakati wa BRELA wa kuimarisha ustawi wa watumishi wake kwa kuzingatia afya bora kama msingi wa utoaji huduma bora kwa wananchi.