Habari
BRELA YATOA GAWIO LA SHILINGI BILIONI 20.4 KWA SERIKALI
BRELA YATOA GAWIO LA SHILINGI BILIONI 20.4 KWA SERIKALI
Dar es Salaam, Juni 10, 2025 — Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), imetoa gawio la Shilingi bilioni 20.4 kwa Serikali kwa mwaka wa fedha 2024/2025, likiwa ni ongezeko la Shilingi bilioni 1.5 kutoka Shilingi bilioni 18.9 zilizotolewa mwaka 2024.
Gawio hilo lilitolewa Ikulu jijini Dar es Salaam na kupokelewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika hafla ya kitaifa ya upokeaji wa gawio na michango kutoka kwa mashirika na taasisi za umma na baadhi ya kampuni binafsi.
Ongezeko hilo la gawio linaashiria ufanisi wa kiutendaji, usimamizi thabiti wa mapato na maboresho ya mifumo ya kidijitali ndani ya taasisi hiyo, asema Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Bw. Godfrey Nyaisa.
Ameongeza kuwa, BRELA imefanikiwa kuongeza mapato kupitia huduma bora kwa wateja na upanuzi wa wigo wa usajili wa biashara na leseni nchini.
Ongezeko la gawio kwa mwaka wa fedha 2024/2025 unatokana na huduma za usajili ambapo hadi kufikia Aprili 2025, BRELA imesajili Kampuni 13,794, Majina ya biashara 23,644, Leseni za Biashara kundi “A” 17,595, Leseni za Viwanda 298, Hataza 37, Alama za Biashara na Huduma 2601. Hiyo ni ishara ya kuimarika kwa uendeshaji wa taasisi na mchango wake kwa maendeleo ya taifa.
Kwa kipindi cha miaka mitano mfululizo, BRELA imechangia gawio la wastani wa Shilingi bilioni 16.8 kila mwaka na hivyo kutambuliwa rasmi kwa kupewa tuzo ya taasisi bora katika utoaji wa gawio kwa Serikali.
Tukio hilo lilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya BRELA, Prof. Neema Mori, na Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Bw. Godfrey Nyaisa.