Habari
WABUNIFU, WASANII NA TAASISI ZANG’ARA KATIKA TUZO ZA MILIKI UBUNIFU ZA IP DAY 2025
WABUNIFU, WASANII NA TAASISI ZANG’ARA KATIKA TUZO ZA MILIKI UBUNIFU ZA IP DAY 2025
Dar es Salaam, Mei 21, 2025 – Serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara imewatunuku wabunifu, wasanii, taasisi na viongozi mbalimbali kwa kutambua mchango wao mkubwa katika kukuza, kulinda na kuendeleza miliki bunifu nchini. Hafla hiyo ilifanyika jijini Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Miliki Ubunifu Duniani (IP Day) ambayo hufanyika kila mwaka duniani kote.
Katika hafla hiyo ya kihistoria, washindi wa makundi mbalimbali walipewa tuzo kwa mchango wao katika maeneo ya hataza, alama za biashara, hakimiliki pamoja na uhamasishaji wa elimu ya miliki ubunifu.
Katika upande wa Hataza, Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST) iliibuka kidedea kwa kuwa taasisi iliyowasilisha maombi mengi ya hataza, ikifuatiwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM). Dkt. Never Daudi Zekeya naye alitunukiwa kwa kuwa mbunifu aliyewasilisha maombi mengi ya hataza kwa kipindi cha miaka mitatu.
Kwa upande wa alama za biashara, kampuni ya Cure Afya Pharmaceuticals Limited iliibuka mshindi baada ya kusajili alama nyingi zaidi ya biashara – ikiwa ni 319 – katika kipindi cha miaka mitano. Aidha, wakala aliyesajili alama nyingi kwa niaba ya wamiliki mbalimbali, ndani na nje ya nchi, pia alitunukiwa.
Katika tuzo za Hakimiliki, msanii maarufu wa muziki Jay Melody (Sharifu Said Msawanga) alitambuliwa kwa kuwa msanii aliyesajili kazi nyingi za muziki Tanzania Bara, huku msanii Saraphina (Sarah Michael Kitinga) akituzwa kama msanii wa kike anayejali na kutambua umuhimu wa hakimiliki. Taasisi ya Tanzania House of Talents (THT) nayo ilitunukiwa kwa mchango wake mkubwa wa kukuza vipaji vya wasanii wachanga.
Zanzibar haikusahaulika. Tuzo ya mfanyabiashara aliyesajili alama nyingi za biashara na huduma ilienda kwa kampuni ya Sub Sahara Trading Partnership, huku Profesa Mohamed Ilyas akitambuliwa kwa mchango wake mkubwa katika muziki wa Zanzibar.
Katika tuzo maalum za utambuzi, kijana mbunifu Pascal Thomas Kija alipokea tuzo kwa ubunifu wake wa kifaa cha kusaidia kupunguza damu kwa wanawake baada ya kujifungua (Safe Belt for PPH), huku Dkt. Never Zekeya pia akitambuliwa kwa bunifu zake za viuatilifu vya kilimo vinavyotumika ndani na nje ya nchi.
Taasisi mbalimbali zilizoonesha juhudi katika kuendeleza elimu ya miliki bunifu kama vile Rive & Co. Advocates, Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBA), COSTECH, SIDO, TWCC, na ARIPO zilitunukiwa vyeti vya utambuzi kwa mchango wao mkubwa.
Pia, majaji waliohusika katika mchakato wa tuzo walitunukiwa vyeti vya utambuzi kwa kazi yao ya kuchambua na kupendekeza washindi kwa uadilifu na weledi mkubwa.
Katika kutambua mchango wa viongozi, Bi. Doreen A. Sinare alitunukiwa tuzo kwa mchango wake akiwa Afisa Mtendaji Mkuu wa COSOTA, huku Bw. Godfrey S. Nyaisa naye akipokea tuzo kwa jitihada zake kama Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA. Viongozi wengine waliotambuliwa ni pamoja na Bw. Victor Michael Tesha, Prof. Neema Mori, na mawaziri wawili: Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi (Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo) pamoja na Mhe. Dkt. Selemani Saidi Jafo (Waziri wa Viwanda na Biashara), ambaye pia alikuwa mgeni rasmi wa maadhimisho hayo.
Tuzo hizo ni sehemu ya jitihada za serikali kuhamasisha ulinzi wa miliki bunifu nchini, kukuza uelewa wa umma kuhusu umuhimu wa hataza, alama za biashara, hakimiliki na mchango wake katika kukuza uchumi wa ubunifu.
"Tunaamini kuwa kwa kutambua na kuthamini michango ya wabunifu wetu, tutajenga msingi thabiti wa maendeleo ya viwanda na uchumi wa ubunifu Tanzania," alisema Dkt. Jafo wakati wa kukabidhi tuzo hizo.
Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali inaendelea kuwekeza katika elimu, sera na miundombinu ya kuimarisha sekta ya miliki ubunifu ili kuhakikisha wabunifu wa Kitanzania wananufaika ipasavyo na kazi zao.