Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni

Tunaipa Uhai wa Kisheria Biashara yako

Habari

VIJANA 1500 WA VYUO WAJENGEWA UWEZO NA BRELA


VIJANA 1500 WA VYUO WAJENGEWA UWEZO NA BRELA

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) imeshiriki kwenye Kongamano la kuwajengea uwezo vijana wa vyuo vikuu na katika kwa kutoa elimu kuhusu urasimishaji wa biashara ikiwemo Usajili wa kampuni, Usajili wa majina ya biashara, na Usajili wa alama za biashara na huduma ili kuhakikisha kuwa biashara zao zinafuata matakwa ya kisheria.


Akitoa mafunzo hayo Bi. Gift Wazingwa - Afisa Usajili kutoka BRELA wakati akiwasilisha mada juu ya umuhimu wa kurasimisha biashara alieleza kuwa, “zipo faida nyingi zitokanazo na kurasimisha biashara zikiwemo, utunzaji wa jina la biashara ama kampuni, kupata ulinzi wa kisheria, kuongeza uwezekano wa kupata wabia, kuongeza fursa za upatikanaji masoko pamoja na upatikanaji wa tenda mbalimbali.”


Bi. Wazingwa aliongeza kuwa, urasimishaji wa biashara unasaidia kuongeza pato la taifa kupitia ada ambazo mfanyabiashara analipa kwa mwaka, hivyo kuendeleza taifa na kuweza kupata huduma mbalimbali katika jamii na kuwezesha ujenzi wa miundombinu ya kuwafikia wafanyabiashara, ikiwemo ujenzi wa masoko na uwekaji wa mazingira wezeshi ya biashara.

Bw. John Minja - Mkurugenzi wa Taasisi ya Piga Kitabu Unity ambao ndiyo waandaji wa Kongamano hilo ameishukuru BRELA kwa kushiriki na kutoa mafunzo hayo yenye lengo la kumwezesha kijana kutumia uwezo wake kudhubutu na kujiendeleza. Bw. Minja amesema kuwa anaamini kila kijana anakitu ambacho amezaliwa nacho hivyo mafunzo haya yataweza kumuongezea ari ya kutimiza ndogo yake.

Aidha Bw. John Minja ameitaka BRELA kushirikiana kwa karibu ili elimu hii inayoitoa iwe endelevu na ijulikane kila mahali, kwa kuwa huduma nyingi za kibiashara kubwa ama ndogo zinahitaji huduma za BRELA.

Mwanafunzi wa Chuo cha Afya Morogoro Musa Maganza alieleza kuwa awali alitaka kuanzisha biashara na alikosa taarifa sahihi kuhusu taratibu za kuanzisha biashara na alieleza, “mafunzo haya yamenifunua sana na ninatarajia kufungua biashara yangu mkoani Geita.”

Kongamano hilo lilikutanisha vijana 1,500 kutoka Vyuo Vikuu na vya kati vilivyopo mkoani Morogoro ikiwemo Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Chuo Kikuu cha Jordan (JUCO) na Vyuo vya kati vikiwemo Chuo cha Afya na Sayansi shirikishi Morogoro, Chuo cha Ardhi Morogoro, Chuo cha Afya cha Mtakatifu Markusi Morogoro.

Shirika la Piga Kitabu Unity limekuwa likiandaa makongamano ya aina hii na kutoa mafunzo mbalimbali kuhusu fursa za kujiendeleza kimasomo, mafunzo kwa wanafunzi ambao wanajiandaa kupata ajira na kujiajiri. Dhima la Kongamano la mwaka huu ilikuwa “IGNITE YOUR LIFE AFTER CAMPUS.’’