Habari
BRELA YAWAFIKIA WAFANYABIASHARA WILAYA YA ILALA
BRELA YAWAFIKIA WAFANYABIASHARA WILAYA YA ILALA
Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), imewahimiza wafanyabiashara katika Wilaya ya Ilala kuwasilisha taarifa za Wamiliki Manufaa wa Kampuni zao (Beneficial Ownership) ili kukidhi takwa la kisheria.
Wito huo umetolewa leo tarehe 02 Disemba, 2024 na Afisa Usajii wa BRELA Bw. Selemani Selemani wakati wa ukaguzi elimishi kwa wafanyabiashara waliokuwa wakipata elimu kuhusu huduma zitolewazo na BRELA maeneo ya Posta jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na wafanyabiashara hao Bw. Selemani amesema zoezi hilo limelenga katika kutoa elimu na kuhimiza kuhusu umuhimu wa kuwasilisha taarifa za Wamiliki Manufaa wa Kampuni (Beneficial Ownership).
“Lengo kuu ni kuwapa elimu wafanyabiashara ambao bado hawajawasilisha taarifa za Kampuni zao ili watekeleze matakwa ya kisheria baada ya usajili”, amesema Bw. Selemani.
Pia ametumia fursa hiyo kuwasikiliza na kupokea changamoto wanazokumbana nazo wakati wa kupata huduma za BRELA kupitia mfumo wa usajili kwa njia ya mtandao .
Ukaguzi huu elimishi utaendelea kufanyika katika wilaya zote za Jiji la Dar es Salaam ambazo ni Ilala, Kinondoni, Temeke, Ubungo na Kigamboni.