Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni

Tunaipa Uhai wa Kisheria Biashara yako

Habari

NYAISA AELEZA HATUA MUHIMU KUWAINUA WABUNIFU KITAIFA NA KIMATAIFA


NYAISA AELEZA HATUA MUHIMU KUWAINUA WABUNIFU KITAIFA NA KIMATAIFA

Na Mwandishi Wetu – Dar es Salaam

Wito umetolewa kwa wabunifu nchini kuhakikisha wanazingatia usajili wa kazi zao, ubora na kujenga chapa imara ili kujinufaisha na kushindana katika soko la kimataifa.

Wito huo umetolewa jijini Dar es Salaam na Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Godfrey Nyaisa, katika maadhimisho ya Siku ya Miliki Bunifu Duniani kwa mwaka 2025.

“Wabunifu wengi bado hawasajili kazi zao na kujikuta wanapoteza kazi zao za ubunifu,” alisema Nyaisa.

Alitoa mfano wa watangazaji wa redio na televisheni wanaobuni vipindi vya kipekee lakini hawavisajili.  “Unakuta mtangazaji wa kipindi cha redio au TV anabuni kipindi kizuri, lakini hakisajili. Akihama kituo, anaacha kipindi chake wakati angesajili angeweza kuhama nacho na kujipatia manufaa zaidi,” alieleza.

Nyaisa alisisitiza kuwa usajili wa kazi bunifu si suala la hiari, bali ni nyenzo muhimu ya kulinda haki na kujiweka katika nafasi nzuri ya ushindani.  “Ni muhimu sana kuzingatia ubora wa kazi za bunifu ili kushindana kimataifa.

Ukitengeneza kitu, kifanye kiwe shindani ndani na nje ya nchi. Hii huongeza thamani ya bunifu na maisha ya mbunifu kiujumla,” alisema.

Kuhusu ujenzi wa chapa (branding), Nyaisa alisema wabunifu wanapaswa kujitangaza zaidi ili kazi na majina yao yatambulike vizuri katika jamii.

“Tangaza brand yako ili hata jina lako likitajwa popote watu waweze kulifahamu vizuri,” alisisitiza.

Mbali na hayo, alishauri elimu ya miliki bunifu ianze kufundishwa mashuleni ili kuwajengea watoto na vijana uelewa wa mapema kuhusu umuhimu wa kulinda na kusajili kazi zao.

“Tukianza kufundisha elimu ya umiliki wa bunifu mashuleni na kutambua wabunifu kupitia tuzo, tutawajenga vijana wenye maono na weledi wa kulinda kazi zao,” alisema.

Kauli ya Nyaisa ni kumbusho kwa wabunifu kuchukua hatua za makusudi kulinda kazi zao, kuziweka katika viwango vya ushindani na kuhakikisha wanajenga chapa zinazotambulika. Hii ndiyo njia pekee ya kuhakikisha ubunifu unaleta tija kwa mbunifu na taifa kwa ujumla.