Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni

Tunaipa Uhai wa Kisheria Biashara yako

Habari

BRELA YATIMIZA AHADI YA KUWALETA WATOTO YATIMA KITUO CHA TUYATA MJI WA SERIKALI MTUMBA


BRELA YATIMIZA AHADI KWA WATOTO WA KITUO CHA TUYATA

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), imetimiza ahadi ya kuwapeleka watoto 100 wa Kituo cha Tulee Yatima Tanzania (TUYATA) kilichopo Magomeni Mwembechai, Dar es Salaam kwenda jijini Dodoma kwa kutumia treni ya kisasa maarufu iitwayo SGR.

Ziara hiyo ya aina yake ni utekelezaji wa ahadi iliyotolewa na Afisa Mtendaji Mkuu Bw. Godfrey Nyaisa Tarehe 22 Machi 2025 wakati wa futari maalum katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani uliomalizika hivi karibuni ikiwa ni sehemu ya juhudi za Taasisi hiyo kurejesha kwa jamii.

Akizungumza kwa niaba ya Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Afisa Habari Mkuu Bi. Joyce Mgaya alisema ziara hiyo inaonesha dhamira ya BRELA katika kusaidia makundi yenye uhitaji maalum.

“Kwa upendo, huruma na nia njema, Afisa Mtendaji Mkuu wetu aliona ni jambo jema kuwapa watoto hawa fursa ya kutembelea makao makuu ya nchi na kujionea miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali,” alisema Mgaya.

Kwa upande wake Mkurugenzi na Mwanzilishi wa kituo cha TUYATA, Bi. Fauzia Jabir aliishukuru BRELA kwa kile alichokiita msaada usiosahaulika.

“Watoto wamefurahi mno, jambo hili halijawahi kutokea. BRELA imefanya jambo kubwa kwa kusimama na watoto hawa wahitaji. Wamehamasika kusoma zaidi baada ya kuona uzuri na fursa zilizopo nchini,” alisema.

Hata hivyo, alieleza kuwa licha ya mafanikio ya kielimu waliyonayo, kituo hicho kinakabiliwa na changamoto kubwa ya makazi kwa watoto yatima, na hivyo kuomba msaada wa ujenzi wa nyumba za makazi kwa watoto na wajane.

Mmoja wa walionufaika na kituo hicho, Ayman Abubakar ambaye pia ni msemaji wa TUYATA, alisema kulea watoto kutoka mazingira mbalimbali si kazi rahisi lakini kwa neema ya Mungu, wanajitahidi kutoa malezi bora na kuwaelekeza katika njia sahihi.

Naye Mudrick Saidi mmoja wa watoto wa kituo cha TUYATA alisema kuwa safari hii imembadilishia fikra na kumpa taswira mpya katika ufahamu wake kutokana na mambo mbalimbali aliyoyaona wakati wa safari na Treni ya SGR.

"Kikubwa kilichonifurahisha na kunishangaza ni namna tulivyo safiri na Treni ya kisasa kutoka Dar es Salaam hadi hapa Dodoma. Nimefurahi kuona maeneo mbalimbali ya Serikali kama vile Bunge, stendi ya mabasi ya saba saba, na Mji wa Serikali wa Magufuli City," alisema Mudrick.

Utimizaji wa ahadi hiyo kwa BRELA ni sehemu moja kati ya mengi ambayo inafanya katika kurejesha kwa jamii kwa kuwafikia wadau mbalimbali wenye uhitaji maalumu.