Habari
BRELA YAPONGEZWA KWA KUTOA ELIMU KWA WAFANYABIASHARA
BRELA YAPONGEZWA KWA KUTOA ELIMU KWA WAFANYABIASHARA
Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), imepongezwa kwa hatua ya kuwanoa wafanyabiashara wa Mwanza kwa kuwapatia elimu ya Usajili wa Alama za Biashara na Huduma kwa kuwa wengi huzalisha na/au kuingiza bidhaa sokoni bila kufahamu umuhimu wa sajili hizo.
Pongezi hizo zimetolewa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Bw. Balandya Elikana, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Amos Makalla, wakati Maafisa wa BRELA walipokwenda Ofisini kwakwe kujitambulisha tarehe 14 Novemba, 2023.
Kaimu Mkuu wa Sehemu ya Hataza Bi Neema Kitala, akimwakilisha Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, ameeleza kuwa Taasisi imedhamiria kuwajengea uwezo wazalishaji na wafanyabiashara wa bidhaa na huduma mbalimbali kwa lengo la kuwawezesha kulinda Alama zao na kuhimili ushindani katika masoko ya ndani na nje, kuaminika na walaji na zaidi kuwaepusha kuingia kwenye migogoro.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti washiriki wa Mafunzo hayo kutoka Wilaya ya Ilemela wameelezea kuridhishwa na huduma za BRELA. Meneja wa Kampuni ya Joasamwe inayozalisha gundi ya karatasi, Bi. Fauzia Ibrahim amesema kuwa walianza uzalishaji baada ya kusajili Kampuni yao, hata hivyo walikumbana na changamoto ya kutumia nguvu kubwa ya kutambulisha bidhaa yao sokoni.
“Bidhaa ya gundi ya karatasi inazalishwa ndani na nje ya nchi na bidhaa hiyo ni nyingi sokoni, kutokana na elimu tuliyopata tutachukua hatua ya haraka kusajili Alama yetu ya biashara ili iweze kujulikana na kutofautishwa na washindani wetu kwakuwa bidhaa yetu ni bora zaidi,” amesema Bi. Ibrahim.
Kwa upande wake Bw. Salum Ramadhani ameeleza kuwa changamoto kubwa waliyonayo ni kutokuwa na ufahamu wa usajili wa Alama za Biashara, kwani walijua usajili ni wa Kampuni pekee, lakini kupitia Mafunzo hayo wamepata uelewa na watasajili Alama za Biashara ambazo zitakuwa na upekee na zenye kutambulisha bidhaa zao.
Naye Bi. Salome Nyakwaka ameishukuru BRELA kwa kutoa elimu ya Alama za Biashara na Huduma kwakuwa wengi walikuwa hawajui umuhimu wa kusajili Alama zao na wengi wanazalisha bidhaa kwa kuweka Alama zenye mfanano bila kufahamu athari ya kutumia Alama hizo.
BRELA inasimamia Sheria za Miliki Ubunifu ambazo ni Sheria ya Alama za Biashara na Huduma pamoja na Sheria ya Hataza. Sheria ya Alama za Biashara na Huduma inalenga kuwalinda wazalishaji wa bidhaa na huduma wanaobuni alama, nembo, michoro, ishara mbalimbali kwa lengo la kutofautisha bidhaa au huduma zao wanapoingiza sokoni, na Sheria ya Hataza inatoa haki ya kipekee ya ulinzi inayompa mbunifu wa bidhaa mpya au mchakato unaolenga kutatua changamoto za katika jamii.