Habari
DKT JAFO AWATAKA WABUNIFU KUSAJILI BUNIFU ZAO BRELA
DKT JAFO AWATAKA WABUNIFU KUSAJILI BUNIFU ZAO BRELA
Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Selemani Jafo amewataka wabunifu wote nchini
kulinda bunifu zao kwa kuzisajili kisheria ili zisichukuliwe na watu wengine na kujinufaisha nazo bila kufuata utaratibu wa kisheria.
Wito huo umetolewa leo katika ziara aliyoifanya ofisi za Wakala wa Usajili wa Biashara na
Leseni (BRELA) jijini Dar es Salaam ili kujionea utendaji kazi na kujifunza namna Wakala
inavyotoa huduma za Sajili mbalimbali.
Akizungumza katika kikao hicho Dkt. Jafo amebainisha kuwa kuna bunifu nyingi ambazo
zinachukuliwa na na watu wengine wanaziendeleza na kujiongezea kipato lakini wale wabunifu hawanufaiki na chochote kwa kuwa hawakuzisajili.
“Ninatoa wito kwa watanzania wabunifu wote kusajili bunifu zenu kupitia BRELA maana taasisi
hii inakazi ya kulinda haki za ubunifu ili kuwawezesha kufaidika na jitihada za ubunifu na hatimaye kuongeza kipato kwa wabunifu na taifa kwa ujumla” amesisitiza Dkt. Jafo
Ameeleza kuwa, Tanzania imesaini mikataba na nchi mbalimbali katika nchi za Jumuiya ya
Afrika Mashariki, Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) pamoja na Soko Huru la
Biashara Afrika (AfCFTA) katika maeneo hayo yote Watanzania wanashiriki katika biashara
mbalimbali hivyo kuna haja kubwa ya wabunifu kutambua haki zao ili zisichukuliwe na wenzetu
hivyo niwaombe Watanzania kusajili bunifu zao.
Amewaelekeza watumishi wa BRELA kuwa wawezeshaji wa Wafanyabiashara kwa kuwasaidia katika kufanikisha kurasimisha biashara zao na siyo kuwa kikwazo. Aidha, amewataka kutumia kanuni na sheria kusaidia biashara kwenda mbele na sheria ambazo zinakwamisha ziwasilishwe ili ziweze kufanyiwa maboresho. Ni muhimu kuelewa jukumu la BRELA ni kujenga misingi na mazingira mazuri ya biashara.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wizara kwa BRELA, Prof. Neema Mori, amesema
kuwa BRELA imedhamiria kuhakikisha mazingira ya ufanyaji biashara nchini yanakuwa bora
zaidi kwa kuwawezesha, kuwarahisishia na kutoa usaidizi wa karibu kwa wafanyabiashara
wanapo rasimisha biashara, kutoa elimu pamoja na kuwahusisha wadau mbalimbali ili wajue
namna.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Bw. Godfrey Nyaisa amesema kuwa kwa
sasa sera ya miliki ubunifu inaelekea kupitishwa na baadae kuwa na sheria ambayo itasaidia
ongezeko kubwa la maombi ya ulinzi wa bunifu hizo ambapo kuna jitihada ambazo BRELA
inaendelea nazo katika kuhakikisha elimu ya miliki bunifu inafahamika kuanzia ngazi ya shule
ya za msingi hadi vyuo vikuu.
Mbali na jukumu la kusajili miliki ubunifu na utoaji wa hataza amesema kuwa BRELA inatoa
ufadhili wa Shahada ya Uzamili ya Miliki Ubunifu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa
watu watano kila mwaka ambapo elimu hii mtu atakayoipata itasaidia katika ukuaji wa sekta ya
miliki ubunifu nchini.